Mbunge Chadema asema Lissu anatosha kuwania urais 2020

Monday January 14 2019

 

By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Jesca Kishoa amesema zawadi pekee ambayo Watanzania wanaweza kumpa mbunge wa chama hicho jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu ni kumuunga mkono katika ndoto zake za kugombea urais mwaka 2020.

Kishoa  ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Januari 14, 2019 katika mkutano wake na waandishi wa habari mjini Dodoma alipoulizwa swali kuhusu afya ya Lissu.

Leo  Lissu ameanza ziara barani Ulaya na atakuwa London, Uingereza ambako amesema ataeleza kwa kina kile alichoandika katika waraka alioutoa kwa ajili ya mwaka huu.

Ziara ya Lissu inaanza baada ya Desemba 31, 2018 kuhitimisha safari ya matibabu aliyoanza Septemba 7, 2017 baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana kwa zaidi ya risasi 30 mjini Dodoma muda mfupi baada ya kutoka kuhudhuria kikao cha mchana cha Bunge.

Lissu ambaye hivi karibuni ameeleza nia yake ya kugombea urais kupitia Chadema, leo ataitikia mwaliko wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Katika maelezo yake leo, Kishoa amemtaka Lissu kutoogopa vitisho kama inavyotokea kwa baadhi ya viongozi wengine ambao hukaa kimya na kuacha kuwatetea wanyonge mara tu wanapokumbana na misukosuko.

“Lissu ni kaka yangu, ni mbunge mwenzangu na kiongozi wangu, mambo ya kuangalia ni kupata baraka za chama lakini anafaa,” amesema Kishoa.

Amesema wakati ukifika atatamani kuona jina la Lissu likipitishwa kuwania urais, kwa maelezo kuwa Watanzania wanajua msimamo wa kiongozi huyo na ndio anayefaa kuwaongoza.

Akizungumzia kuhusu ziara za Lissu katika mataifa mbalimbali, amesema ni haki kwa mbunge huyo kwa kuwa anaeleza kilichompata kwani wengi hawajui ukweli wa jambo hilo.

Katika waraka wake huo alioutoa Januari 5, 2019 Lissu alitaja matukio ya uvunjifu wa haki za binadamu huku pia akihoji sababu ya Bunge kutogharamia matibabu yake, mambo ambayo pia amesema kwamba atayaeleza katika ziara yake hiyo.

Waraka huo wenye kichwa cha habari ‘Mwaka mpya 2019, Mwaka wa kurudisha demokrasia, haki za binadamu na utu wetu Tanzania’ umegusia pia masuala ya haki za binadamu yakiwamo matukio ya utekaji, mauaji na mashambulio ya kudhuru mwili.

Mbali na kudai gharama za matibabu, Lissu amelalamika kutotembelewa na Spika Job Ndugai wala watumishi wa Bunge tangu alipolazwa hospitali licha ya kuwapo kwa ahadi hiyo.

Advertisement