Mbunge Chadema ataka kujua kama kodi ya kichwa imerudi Tanzania

Tuesday June 25 2019

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Lucia Mlowe ameihoji Serikali ya Tanzania iwapo imerudisha kodi ya kichwa kwa utaratibu wa uuzaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo wadogo.

Mlowe ameyasema hayo bungeni jana Jumatatu Juni 24, 2019 wakati akichangia mapendekezo ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni.

Alisema mkoani Njombe wamesomewa barua makanisani kuwa watu wote wanatakiwa kuwa na vitambulisho vya wafanyabiashara ndogo ndogo.

Alitoa mfano wa watu wanaotakiwa kuwa na vitambulisho hivyo ni pamoja na  wanaowasaidia mama lishe kuosha vyombo, walima bustani na mafundi ujenzi.

“Naomba kujua hivi kodi ya kichwa imerudi? Kwa kweli inasikitika wananchi wamechanganyikiwa. Waziri atakapokuja kuhitimisha atuambie ni watu gani wanaopaswa kuwa na vitambulisho?,” alihoji.

Aidha, Mlowe alisema mashine za Kielektroniki ni mbovu zinaharibika kila mara na kwamba kila inapoharibika mfanyabiashara anatakiwa kutengeneza kwa Sh150,000.

Advertisement

“Kwanini isitafute kampuni inayoweza kutengeneza mashine imara, utakapokuja hapa mheshimiwa waziri ulitolee ufafanuzi hili,” alihoji.

Advertisement