VIDEO: Hivi ndivyo Mbunge Jaguar alivyokamatwa na polisi nje ya bunge

Muktasari:

Ni Charles Kanyi maarufu Jaguar aliyetaka wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda waliopo jijini Nairobi wakamatwe na kupigwa

Nairobi, Kenya. Mbunge wa Starehe nchini Kenya, Charles Kanyi maarufu Jaguar anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kutoa kauli za chuki dhidi ya wafanyabiashara wa Tanzania na Uganda waliopo jijini Nairobi.

Kwa mujibu gazeti la Daily Nation, mbunge huyo alikamatwa leo Jumatano June 26, akiwa katika viwanja vya bunge alipokuwa akihudhuria vikao vya Bunge la Bajeti.

Jumatatu iliyopita mbunge huyo ambaye ni mwanamuziki wa miondoko ya Hip pop alionekana katika video fupi ambayo ilisambaa katika mitandao ya kijamii akizungumza na wafanyabiashara wa jijini humo na kuwaeleza kuwa hawatokubali watu wa nje waje kufanya biashara nchini mwao.

''Wakenya ni sharti wafanye biashara zao bila kushindana na watu kutoka mataifa mengine. Raia wa Pakistan wametawala biashara za kuuza magari nchini humu, Watanzania na Waganda wanatawala katika masoko yetu. Tunasema imetosha iwapo hawatarajeshwa nyumbani katika saa 24 tutawashika na kuwapiga na hatuogopi mtu yeyote,” alisisitiza mbunge huyo.

Tangu kipande hicho cha video kionekane katika mitanao ya kijamii, kimeibua sintofahamu ambako wabunge wa Tanzania jana walitoa hoja wakitaka Bunge litoe tamko la kulaani kitendo hicho ikiwa ni pamoja na kumtaka mbunge huyo kuomba radhi.

Hoja hiyo ilimuibua Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa na kuwaomba Watanzania kuwa watulivu wakati Serikali ikishughulikia suala hilo.

Waziri Majaliwa alisema tayari hatua za awali zimefanyika ikiwamo ni pamona na kuzungumza na balozi wa Kenya nchini Tanzania ili kufahamu iwapo ni kauli ya Serikali.

Hata hivyo, baadaye jioni Serikali ya Kenya ilitoa taarifa ikilaani kitendo kilichofanywa na mbunge huyo na kusisitiza kuwa haihusiki kwa lolote na kauli hiyo.