Mbunge achambua ndege ya Serikali, ahoji iliko airbus

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Devota Minja akichangia bungeni mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Devota Minja amehoji kuhusu faida na ilipo ndege ya Airbus.

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Devota Minja amehoji Serikali ni wapi ilipo ndege ya Airbus iliyoingia nchini hivi karibuni na kufanya shughuli kusimama kwa ajili ya mapokezi.

Akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa fedha 2019/20, leo Ijumaa Aprili 05, 2019 Minja amesema jana Waziri Mkuu amesema wamenunua ndege nne bombardia  ambazo zimegharimu zaidi ya Sh280 bilioni.

Amesema kuwa juzi wameelezwa matengenezo ya ndege yamegharimu Sh14 bilioni na kuhoji hivi ni kweli zinatengeneza faida ndege hizo.

“Airbus moja ambayo ni takribani Sh200 bilioni iko wapi tuliambiwa kuwa italeta watalii kutoka Marekani? Hivi ndege hii iko wapi? Kwanini hatuioni ikifanya kazi?” amehoji Minja.

Minja amesema kwa sababu wakisoma katika mitandao wanasema kuwa imeuzwa Kenya mara iko kwenye matengenezo, mara iko gereji mara iko inapakwa rangi.

“Ndege iliyokuja juzi shughuli zote zilisimama kwa sababu ya ndege moja ambayo imekuja nchini leo hatuelewi kwamba hadi sasa imezalisha shilingi ngapi? Zipo taarifa inaonekana inabeba nyama kutoka Mwanza, tunataka tuambiwe kwa sababu zimenunuliwa na fedha za Watanzania,” amesema.

Amehoji ziko wapi ndege hizo zibebe watalii ziongeze pato la nchi na zinafanya kazi gani sasa?

“Tunahitaji fedha za Serikali zitumike vizuri badala ya kuleta ndege tangu miezi mitatu ime ‘ground’ badala ya kwenda nje ikafanye hayo Serikali imesema matokeo yake tunasikia katika mitandao tungependa kufahamu ni kitu gani specific kinaendelea,” amesema.

Aidha, amesema hivi karibuni wamesikia kuhusu ndege ya fokker ambayo teknolojia yake ni ya mwaka 1985 imeanza kuongezewa siti kwa ajili ya kubeba abiria na kuonya siasa zisiwekwe katika mambo ya usafiri wa anga.

“Ndege hizi ambazo sasa hivi hazitengenezwi tena, teknolojia yake ni ya zamani tunaenda kuchomelea viti tunaongeza abiria na kubeba mizigo watu watabeba samaki  kutoka Mwanza, tusicheze na maisha ya wananchi,” amesema.

Soma zaidi:

Hata hivyo, Naibu Waziri wa Ujenzi,  Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kuandikwa amesema hauwezi kurusha ndege yenye abiria bila ya kuthibitishwa viwango vyake vya usalama ambavyo viko kimataifa.

“Kwa maana hiyo zoezi linaloendelea limezingatia standard za kimataifa, linazingatia usalama na mambo yote hayo yanazingatiwa,” amesema.