Mbunge afananisha vitambulisho vya machinga na kodi ya kichwa

Mbunge wa Mbozi, Pascal  Haonga akichangia bungeni mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Mbunge wa Mbozi (Chadema) Pascal Haonga ametaka ufafanuzi kuhusu mtaji ambao analazimika kuwa nao mjasiriamali  mdogo ili awe na sifa ya kupewa vitambulisho.

Dodoma. Mbunge wa Mbozi (Chadema), Pascal Haonga amehoji Serikali ni kima gani cha chini ambacho mjasiriamali mdogo anatakiwa awe nacho ili awe na sifa za kupewa kitambulisho kwa sababu mpango huo ni kama kodi ya kichwa imerudishwa.

Amehoji hayo bungeni leo Jumatatu Aprili 15, 2019 wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma) na Tamisemi kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Amesema Rais John Magufuli aliposema wananchi wanaotakiwa kupata vitambulisho ni wale wenye mtaji wa kuanzia milioni nne na kushuka chini.

“Alikuwa anamaanisha kushuka chini hadi mtaji wa kiasi gani hadi Sh500 kwa sababu kuna wakinamama  ambao wanauza nyanya wana mtaji wa Sh 1,000  anatakiwa alipie Sh20,000,”amesema.

“Mama mwingine anauza nyanya chungu ana mtaji wa Sh500 anaambiwa anunue, ni Sh4 milioni hadi shilingi ngapi. Tender (zabuni) ilitangazwa kupata huyo anayetengeneza vitambulisho na kama ilitangazwa ni nani aliyeshinda,” amesema.

Amesema  maana yake kama kuna makosa yaliyofanyika visije vikawa ni dili la mtu na wabunge wakatumika kama rubber stamp kupitisha jambo la mtu. “Na kama kulikuwa tender ni nani aliyeshinda tenda hii. Kule Mlowo, Mpangala wakinamama wanahangaika  sana na hii imekuwa kama kodi ya kichwa imerudishwa leo,”amesema.

Amesema mama anauza nyanya anaambiwa alipe Sh20,000, baba anauza miwa anaambiwa alipe Sh20,000,  mtoto anauza bamia anaambiwa Sh20,000 na hivyo kufanya nyumba moja kulazimika kutoa Sh80,000.

“Hii ni zaidi ya kodi ya kichwa watuambie kodi ya kichwa hatutakubali kodi hiyo irudishwei. Mliahidi kutoa Sh50 milioni kila kijiji lakini badala ya kupeleka mmeenda kudai Sh20,000,” amesema.

Amesema kama Sh50 milioni kwanini haikutolewa badala yake wanadai pesa Sh20,000 nchini nzima.

Amesema kwamba kama imerudishwa kodi ya kichwa wabunge hawatakuwa tayari kukubaliana na jambo hilo.