Mbunge aibua kasoro kituo cha Misugusugu, waziri amjibu

Monday April 15 2019

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Mary Muro amehoji ni lini Serikali itahamisha Kituo cha Misugusugu Check Point kwani kimekuwa kero kutokana na vumbi linalosababishwa na miundombinu mibovu na hivyo watu kuugua ugonjwa wa Kifua Kikuu.

“Kwanini Serikali haifikirii kabla ya kufanya mradi maana vumbi la pale linawapa watu TB (kifua kikuu). Ni mkakati gani wa haraka unafanyika kuyaondoa malori hapo?” Amehoji bungeni leo Jumatatu Aprili 15 mwaka 2019.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji amesema Serikali inatekeleza mradi wa kituo cha pamoja cha ukaguzi wa mizigo ili kuwezesha mamlaka za ukaguzi kufanya kazi ya ukaguzi katika eneo moja.

“Sambamba na mradi wa mizani ya ukaguzi mizigo iliyopo vigwaza mkoani Pwani. Taasisi zinazohusika katika mradi huu ni pamoja Tanroads (Wakala wa Barabara Nchini), polisi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),”amesema.

Amesema TRA ipo katika hatua za awali za kujenga na kusimika mifumo ya ukaguzi katika eneo la mradi lililopo Vigwaza.

Amesema hivyo kituo cha ukaguzi wa mizigo kitahamishwa kutoka Misugusugu kwenda Vigwaza mara baada ya kazi ya kusimika mifumo kukamilika.

Kuhusu kufikiria kwa Serikali kabla ya kuanza mradi, Dk Kijaji amesema kuwa siku zote Serikali imekuwa ikifikiria na hata sasa inafikiria.

Amesema ndio maana Serikali sasa inatekeleza mradi huo wa Vigwaza kwa Euro milioni 23.

Amesema mradi wa ujenzi wa kituo kama cha Vigwaza unatekelezwa katika maeneo ya Manyoni na Nyakamazi.

Amesema mkakati wa Serikali ni kukamilisha kituo hicho cha Vigwaza kwa wakati uliopangwa ambacho kitarahisisha udhibiti wa mapato.

Amewataka Watanzania kujiuliza pale malori ya mizigo yanaposhusha mizigo kijijini badala ya mijini.

Advertisement