Mbunge mmoja kati ya watatu Chadema aeleza sababu za kutosusia kikao cha Bunge

Wabunge wawili wa Chadema pekee waliobaki kwenye ukumbi wa Bunge kufuatia wengine kutoka ukumbini wakiashiria kupinga adhabu ya kutohudhuria mikutano mitatu aliyopewa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, jijini Dodoma leo. Wabunge hao ni Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali na Mbunge wa Viti Maalumu, Annatropia Loikila. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Wabunge wa Chadema waliobaki ukumbini wakati wenzao wakitoka nje ni, Peter Lijualikali (Kilombero), Anatropia Theonist na Mary Muro (viti maalum).

Dodoma.  Wabunge watatu wa Chadema wameeleza sababu za kubaki ndani ya ukumbi wa Bunge licha ya wabunge wenzao wa chama hicho kususia kushiriki kikao cha leo wakipinga Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kusimamishwa kushiriki mikutano mitatu ya chombo hicho cha kutunga sheria.

Leo Spika Job Ndugai aliagiza wabunge wa Chadema na baadhi wa CUF waliosusia uamuzi huo kwa kutoka nje ya ukumbi kutorejea tena ndani kwa siku ya leo huku akiagiza pia wasihojiwe na wanahabari na wakitaka kufanya hivyo iwe ni nje ya eneo la viwanja vya Bunge.

Wabunge hao ambao Ndugai wakati kikao hicho kikiendelea leo mchana alisema hawakuungana na wenzao kutoka nje ni Peter Lijualikali (Kilombero), Anatropia Theonist na Mary Muro (wote viti maalum).

“Sisi tulichelewa kuingia bungeni na wakati ishu inafanyika hatukuwepo, Spika alisema walioondoka wasirudi na leo tulikuwa tunasoma hotuba ya upinzani bungeni,” amesema Lijualikali.

“Tulirudi, hasa mimi kwa ajili ya kusoma bajeti na nilirudi kwa maagizo na baraka zote za kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni (Freeman Mbowe)  na alinikabidhi hotuba yetu (huku akionyesha hotuba hiyo).”

Alisema Mbowe alishindwa kurejea kusoma hotuba hiyo kwa kuwa Ndugai aliagiza wasirejee bungeni baada ya kutoka nje ndio maana alimuagiza yeye.