VIDEO: Mbunge wa Chadema amvaa Polepole

Muktasari:

Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Upendo Peneza amemvaa bungeni Katibu Mwenezi wa CCM, Humphery Polepole, kuwa anawadhalilisha wabunge wa viti maalumu.

Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Upendo Peneza amemvaa Katibu Mwenezi wa CCM, Humphery Polepole, kuwa amewadhalilisha wabunge wa viti maalumu wanaotokana na chama chake kuwa wamepata nafasi hizo baada ya  kufanya ngono na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Peneza ameyasema hayo jana Jumatano Aprili 17, 2019   akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2019/20.

Amesema wabunge wa viti maalumu wapo kwa mujibu wa Katiba lakini kuna kitu kibaya kilianza kutokea ndani ya Bunge na kwamba, viongozi wa Bunge wanapokaa kuendesha Bunge wamekuwa wakikemea tabia hiyo aliyoita ni ya kipuuzi.

“Lakini sasa tabia hiyo inaendelea huko nje,  Humphrey Polepole, Katibu wa Uenezi wa CCM amesimama na kusema wabunge wa Chadema wanapatikana mpaka wapitiwe na mwenyekiti wao,” amesema.

Amesema ifike wakati watu watambue huo ni udhalilishaji ambao hauruhusiwi na sheria za Tanzania na kwamba, Polepole amefanya kazi katika taasisi za Serikali muda mrefu.

“Sasa kama hata hatambui haki za kikatiba ni aibu kwa Chama cha Mapinduzi kuwa na mwenezi anayedhalilisha wanawake… lakini ifike mahali nafasi walizonazo na vyeo walivyonavyo viheshimiwe,” amesema.

Amesema ni aibu kwa kiongozi kusimama na kusema kuwa nafasi ya mwanamke kisiasa inatokana na ngono.

“Tunawajengea watoto wetu fikra mbaya, hakuna tena jitihada ila jibu pekee waende wakafanye ngono watapata nafasi,” amesema.

Peneza ameiomba utaratibu halisi wa upatikanaji  ujulikane ili kuondoa uchungu na matusi yanayojengeka.

Amesema ifike wakati mabadiliko ya Katiba yafanyike ambayo itaweka utaratibu wa wanawake kugombea viti maalumu ili kujenga heshima ya mwanamke.

Mbunge huyo ametoa mfano wa nchi ya Uganda kwamba wabunge wa viti maalumu hupigiwa kura.

Amesema faida ya utaratibu huo ni kutoa fursa ya uwajibikaji wa wabunge kwa wananchi waliowachagua.

“Utaratibu huu unawezesha wananchi kumwajibisha mbunge ambaye analipwa kupitia kodi zao,” amesema.