Mchakamchaka wa ruzuku shule za msingi 2017/18

Takwimu za Tamisemi zinaonesha Shule ya Msingi Mbuyuni iliyopo Korongwe Tanga yenye wanafunzi 17 ikiwa miongoni mwa shule zenye wanafunzi wachache zaidi, ilipata wastani wa Sh7,338.1 kila mwezi sawa na Sh88,044.6 kwa mwaka. Sh 5,179.1 ndio wastani wa fedha aliyopata kila mwanafunzi kwa mwaka wa fedha 2017/18.

Shule hii ipo katika Kata ya Mkalamo, Tarafa ya Mombo kilomita 70 kutoka Korogwe mjini. Kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo, nauli mpaka shuleni haipungui Sh8,000 kwa usafiri wa kawaida ikiwa ni kwenda pekee na mara mbili zaidi kurudi.

Mwananchi imefanikiwa kufika shuleni hapo na kukuta wanafunzi kadhaa wakicheza nje ya majengo mawili chakavu yaliyoungana. Pembeni kama mita 50 upange mmoja kuna nyumba chakavu zaidi ya 80 zilizo kwenye mpangilio, zikionekana ni kama nyumba za kota kwa kuwa eneo hilo limepakana na mashamba ya mkonge.

Mwananchi limezungumza na walimu kuhusu changamoto wanazozipata wao na wanafunzi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Francis Shechambo anasema changamoto kubwa ni fedha chache za ruzuku wanazozipata kutoka serikalini.

Mwalimu huyo anasema fedha wanazopata wastani wa Sh7,200 kwa mwezi ni za wanafunzi 17 waliokuwepo mwaka 2018 ingawa sasa wameongezeka na kufikia 32 na wanatarajia watafika 40 kwa kuwa usajili wa wanafunzi wa darasa la kwanza kwa mwaka huu haujakamilika.

Kutokana na uchache wa fedha hiyo anasema analazimika kuiacha benki kwa mwaka mzima ili akiitoa mara moja isaidie katika baadhi ya maeneo.

“Nilitoa 2016 mara moja na 2017, sijaitoa karibu mwaka sasa naamini itakua imefika angalau Sh85,000. Naandaa bajeti ili nikaichukue,” asema.

Mwalimu mkuu anaongeza kuwa kutokana na uchache wa fedha hizo huku kukihitajika matumizi ya kila siku analazimika kutumia fedha yake binafsi kununua chaki na makapeni pale zinapoisha.

“Huwezi kuacha kufundisha kisa chaki nalazimika kutoa fedha yangu kidogo au niazime vifaa ambavyo tutavirudisha tutakapopata,” anasema na kuongeza kuwa uchache wa fedha za utawala unasababisha kutohudhuria vikao vya mara kwa mara vinavyofanyika wilayani na kulazimika kupata taarifa kwa walimu wa shule za jirani.

Kwa upande wake Mwalimu Maria Makadi anayefundisha shuleni hapo anaitaja changamoto nyingine ni kukosa vitabu kwa baadhi ya madarasa kutokana baadhi ya madarasa kutokuwa na wanafunzi katika baadhi ya miaka.

“Mwaka 2018 hatukuwa na darasa la tano, hivyo darasa la tano la mwaka huu linakosa vitabu kwa sababu taarifa za maombi ya vitabu zilikwenda kwa wanafunzi waliokuwepo mwaka uliopita” alifafanua na kutaja changamoto nyingine ni kukosa mahitaji ya muhimu yeye kama mwalimu kwani eneo hilo halina huduma nyingi za kijamii kama maji, zahanati na umeme.

Shule hiyo ina wanafunzi watatu wa darasa la saba na haina darasa la sita, lakini pia wanafunzi wa darasa la kwanza bado hawaajaanza kusajiliwa kutokana na mwamko mdogo wa wazazi katika maeneo hayo.

Miongoni mwa wanafunzi wa shule hiyo, Iddi Mtana anayesoma darasa la saba na kuishi katika moja ya nyumba za kota, anasema anashukuru ushirikiano anaoupata kutoka walimu wake kwani licha ya uchache wao wanafundisha kwa bidii.

Mwanafunzi mwingine, Jailosi Simoni anasema shulen iko mbali na makazi yao huku wazazi wakiwa hawana uwezo wa kumpatia mahitaji yote ya jambo linalomuweka katika wakati mgumu kimasomo.

Mzazi wa Iddi Ashura Chande, anasema licha ya ugumu wa maisha anashukuru ushirikiano wa walimu kwani wakati mwingine anapokosa fedha za kununua mahitataji ya wanae walimu wamekua wakiwasaidia.

Shule nyingine yenye wanafunzi wachache ni Shule ya Msingi Wami Vijana iliyopo Mvomero, Morogoro ikiwa na wanafunzi wanne pekee katika mwaka huo wa

fedha ilipata Sh20,716.28 ikiwa ni wastani wa Sh1,726.22 kila mwezi. Hii ina maana kuwa kwa mwaka mzima mwanafunzi mmoja alipata Sh5,179.1.

Katika orodha ya shule hizo ipo pia Kingupira iliyopo Rufiji, Pwani yenye wanafunzi tisa ambapo kwa wastani ilipata Sh3,883.99 kila mwezi sawa na Sh46,611.8 kwa mwaka sawa na mwanafunzi mmoja alipata Sh5,179.1.

Shule zinazopata fedha nyingi

Shule ya Msingi Ludete ndiyo shule iliyopata wastani wa fedha nyingi zaidi kila mwezi. Kati ya Julai 2017 na Juni 2018, shule hiyo ilipata kati ya Sh2,865,295.58 na Sh2,864,874.11 kila mwenzi sawa na Sh34,378,826.42 kwa mwaka huo wa fedha.

Shule hiyo iliyoko wilayani Geita ina wanafunzi 6,616 na kila mwanafunzi alipata wastani wa Sh5,196.3 kwa mwaka.

Mwananchi iliitembelea shule ya Ludete na kubaini kuwa iligawanywa na kuanzishwa shule nyingine hivyo idadi ya wanafunzi walipungua mpaka kufikia 5,941 Januari 2019, ukilinganisha na 6,616 waliokuwepo kabla.

Hatua hiyo ilisababisha wastani wa fedha za ruzuku kupungua mpaka Sh2,266,469.22 kwa mwezi sawa na Sh381.49 kwa mwanafunzi kila mwezi. Hii inaifanya shule hiyo kuwa miongoni mwa shule ambazo mwanfunzi anapata Sh4577.95 kwa mwaka ikiwa ni wastani mdogo miongoni mwa shule nyingi.

Shule hiyo inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo upungufu mkubwa wa madarasa kwani ina madarasa 17 pekee na kufanya darasa moja kukaa kati ya wanafunzi 250 hadi 300.

Akizungumza na gazeti hili mwalimu mkuu wa shule hiyo, Ngoso Kurwa anasema Serikali kwa kushirikiana na wazazi walijenga shule mpya na kuwagawanya wanafunzi ambapo moja ya tatu walihamia shule ya Msufini lakini bado Ludete imeendelea kuwa na mlundikano.

Anasema hadi sasa ameandikisha wanafunzi 884 wa darasa la kwanza na bado uandikishaji unaendelea, hivyo kufanya fedha hiyo kuwa chache zaidi.

Kurwa anasema kutokana na wingi huo wa wanafunzi darasa la kwanza pekee wanatumia madarasa manne na kwamba ili wanafunzi 5,941 waweze kusoma wamegawanywa katika makundi mawili kwa kusoma nusu siku.

Mwalimu Kurwa anasema kutokana na idadi hiyo sasa hahitaji madarasa mapya na ukarabati pekee bali inahitajika shule mpya kwani kanuni ya elimu inataka shule kuwa na wanafunzi 1,200 idadi ambayo katika shule hiyo imevukwa zaidi ya mara nne.

Anasema kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi darasani, uelewa wao umekuwa mdogo licha ya jitihada zinazofanywa na walimu kufundisha.

Naye mwalimu Shija George anaefundisha darasa la 5B, anasema wanafunzi wanapokuwa wengi darasani sio rahisi kuwafundisha na kuwaelewa.

George anasema ili mwanafunzi aweze kuandika analazimika kusimama kwa kuwa waliokaa nyuma hawaoni ubaoni na wakati mwingine hulazimika kusimama juu ya dawati ili waweze kuandika.

“Tunaomba miundombinu na vifaa vya kufundishia viongezwe. Mwalimu mmoja anavipindi vinne kwa siku unawafundisha watoto 300 kusahihisha hayo madaftari ni kazi sana kwa kweli ni ngumu lakini hatuna jinsi,” anasema George.

Shule zinazofuata ni Majimatitu na Mbande zilizopo katika Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam. Wanafunzi wa shule hizo walipata wastani wa Sh5,196.3 na Sh 5,219.5 kila mmoja kwa mwaka huo.

Majimatitu yenye wanafunzi 6,406 ilipokea Sh33,436,231.3 kwa mwaka huo wa fedha sawa na kati ya Sh2,786,113.8 na Sh2,786,325.29. Shule ya Mbande yenye wanafunzi 6,274 ilipata Sh32,493,636.18 ikiwa ni kati ya Sh2,708,174.82 na Sh2,707,776.47 kila mwezi. Shule hizo tatu ndizo zenye wanafunzi wengi zaidi.

Mwananchi iliitembelea shule ya Majimatitu na kubaini kuwa idadi ya wanafunzi imeongezeka hadi kufikia 7,190 January 21, mwaka huu.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Omary Muyenjwa anasema kuwa idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa imekuwa ikiongezeka kila wiki wengine wakiwa ni wale wanaohamia huku mwisho wa usajili ukiwa ni Machi.

Licha ya idadi hiyo kubwa ya wanafunzi fedha ya ruzuku inayopokea shule hiyo ni ile ile ambayo waliiwasilisha kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 2018. Shule hiyo ambayo wanafunzi wake wamegawanyika sehemu tatu ikiwemo kitengo cha memkwa chenye wanafunzi 191 na wanafunzi maalumu 50 inapokea Sh3,529,587.89.

Fedha hizo zimegawanywa kwa wanafunzi wa kawaida wanaopata Sh2,929,587.89, ikiwa ni wastani wa Sh410.3 kwa mwanafunzi kwa mwezi na Sh4,923.7 kwa mwaka. Wanafunzi maalumu wanapata Sh600,000 wakati wanafunzi wa memkwa hawapo kwenye kundi la wanaopokea fedha.

Mwalimu Muyenjwa aliliambia Mwananchi kuwa idadi kubwa ya wanafunzi imekuwa na changamoto katika ugawaji wa fedha za ruzuku ambazo ni chache huku akiongeza kuwa hii inawafanya walazimike kukopa.

Akionesha chati iliyokuwa na deni la Sh1.09 milioni ikioredhesha ununuzi wa vifaa vya usafi kama fagio, kuhifadhia takataka na vile vya kufundishia kama chaki.

“Tunaliazimika kukopa kwa kuwa shule inabidi iendeshwe. Kama chaki zimeisha inabidi tuangalie namna ya kuzipata. Mwishoni utaulizwa kwa nini walimu hawakufundisha na huwezi kutoa sabau eti chaki ziliisha,” anasema.

Mwalimu huyo anaongeza “madarasa 47 tuliyonayo ni machache sana zinahitajika fedha za ujenzi wa madarasa mengine, lakini pia wingi wa wanafunzi unasababisha uharibifu wa haraka wa miundombinu”.

Wastani wa ruzuku kwa mwanafunzi

Kwa mujibu wa takwimu za Tamisemi katika shule 16,088 za Serikali nchini wastani wa fedha alizopata mwanafunzi mmoja ni Sh5,207.55 katika kipindi cha Julai 2017 na Juni 2018 sawa na Sh433.96 kwa mwezi kwa mwanafunzi.

Mwanafunzi mmoja kwa mwaka anatakiwa kupata ruzuku ya Sh10,000 ambayo inagawanywa kwa asilimia. Asilimia 60 ambayo ni Sh6,000 inakwenda moja kwa moja shuleni na asilimia 40 ambayo ni Sh 4,000 inakwenda Tamisemi kwa ajili ya vitabu.

Sh6,000 inayokwenda shuleni imegawanyika katika asilimia zifuatazo. Asilimia 30 (vifaa vya kufundishia), 30 (ukarabati shuleni), 20 (mitihani), 10 (utawala) na 10 ya mwisho (michezo).

Kwa maana hiyo idadi ya wanafunzi milioni 10.37 walipata asilimia 86.8 pekee ya rukuzu iliyokuwa ikifika shuleni kati ya Sh6,000 iliyopangwa na Tamisemi kwa kila mwanafunzi kwa mwaka (Sh500 kwa mwezi).

Asilimia 96.9 ya shule hizo (15,555) zinapata wastani wa Sh5,179.1 kwa mwaka ikiwa ni wastani wa Sh431.6 kwa mwezi.

Shule zenye wanafunzi waliopata wastani mdogo zaidi wa fedha

Shule ya Msingi Mafumbo iliyopo mkoani Kagera katika Manispaa ya Bukoba ndiyo inayopokea wastani mdogo zaidi wa fedha za ruzuku kwa mwanafunzi mmoja kwa kupata Sh4,363.6 kwa mwaka ikiwa ni wastani wa Sh363.6 kwa mwezi.

Shule hiyo ilikuwa na wanafunzi 2,150 na iliopokea Sh9.38 milioni katika kipindi cha mwaka mmoja badala ya Sh12.9 milioni. Ilipokea Sh51,366.4 kati ya Julai na Agosti 2017 na Sh927,959.35 Septemba 2017 na Juni 2018.

Inayofuata ni Shule ya Msingi Igoma, iliyopo Mwanza mjini ambapo wanafunzi wake walipata wastani wa Sh4,606.7 kati ya Julai 2017 na Juni 2018 ikiwa ni wastani wa Sh383.9 kwa mwezi.

Shule hiyo ina wanafunzi 2,801 na ilipokea Sh12,903,532.6 katika kipindi sawa na Sh620,622.02 kila mwezi.

Wanafunzi waliopata zaidi ya Sh 6,000

Kati ya shule zote ni shule 36 pekee zilizokuwa zikipata wastani wa zaidi ya Sh 6,000 kwa mwezi. Miongoni mwa hizo ni Shule ya Msingi Mitindo iliyopo wilayani Misungwi, Mwanza.

Shule hiyo yenye wanafunzi 1,201 inayopokea Sh6,201.1 kwa mwanafunzi kwa mwaka ikiwa ni wastani wa Sh516.8 kwa mwanafunzi kwa kila mwezi, takribani Sh620,574.9 hupokewa na shuleni hapo kila mwezi.

Shule tano ambazo wanafunzi wake huneemeka kwa kupata zaidi ya Sh 10,000 kwa mwaka ni Ruvu Remit iliyopo Simanjiro, Manyara ambayo wanafunzi hupata Sh10,887.1 kwa mwaka na shule ya Laalarik ya Kiteto, Manyara Sh13,485.2.

Nyingine zinazopata zaidi ya Sh20,000 kwa mwanafunzi ni Buirigi Blind ya Chamwino, Dodoma Sh20,543. 7, Makame iliyopo Kiteto, Manyara Sh21,586.81 na Ndedo pia ya Kiteto wanafunzi wake hupata wastani wa Sh288,475.5 kwa mwaka.

Mwananchi ilifika katika shule ya Ndedo na kubaini inwanafunzi baadhi wanaokaa bweni na wengine wa kutwa na ilikuwa na wanafunzi 770, tofauti na wanafunzi 10 walioorodheshwa kwenye takwimu za Tamisemi.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo Philip Bajutu anasema shule hiyo yenye walimu sita inapokea wastani wa Sh249,000 kwa mwenzi. Hii inamaana kuwa mwanafunzi mmoja anapata wastani wa Sh3,880.5 kwa mwaka. Mwalimu Bajutu anasema ”uchache wa fedha za ruzuku unawalazimu kukopa kweye maduka pale wanapoishiwa kwa ajili ya mahitaji muhimu kama kalamu, daftari na chaki”.

Anasema kutokana na mwitikio wa wazazi juu ya elimu bure, wanafunzi wengi wanahudhuria shuleni na kusababisha mrundikano madarasani.

“Kuna baadhi ya wanafunzi wa darasa la kwanza hadi la nne wanakuwepo wengi ambapo unakuta darasa moja lina wanafunzi 110 au zaidi,” anasema.

Katika shule ya Makame ambayo pia ni ya bweni, mwalimu mkuu wa shule hiyo iliyopo, kata ya Makame wilayani Kiteto, Danstan Kimu anasema shule yake ina wanafunzi 649 wakiwamo zaidi ya 100 wa kutwa.

Mwalimu Kimu Anasema shule hiyo ilikua ikipata ruzuku ya Sh214,000 kwa mwezi ila tangu Desemba mwaka jana wanapokea Sh373,000 kwa mwezi. Hii inamaana mwanafunzi mmoja wa shule hiyo anapata wastani wa Sh6,896.7 kwa mwaka ikiwa ni zaidi kidogo ya Sh6,000 inayotakiwa.