Mchakato ujenzi wa daraja la juu Gerezani Dar waanza

Muktasari:

  • Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad), Patrick Mfugale amesema kampuni ya Sumitomo Mitsui itaanza hivi karibuni kujenga daraja la Gerezani  litakalogharimu Sh 25.28 bilioni.

Dar es Salaam. Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad), Patrick Mfugale ameahidi kuisimamia vyema kampuni ya ujenzi ya Sumitomo Mitsui ya Japan itakayojenga daraja la Gerezani jijini Dar es Salaam ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati.

Mbali na ujenzi wa daraja hilo, kampuni ya Sumitomo Mitsui imejenga pia daraja la juu la Mfugale lililopo eneo la Tazara katika barabara la Nyerere.

Mfugale ametoa kauli hiyo leo wakati wa hafla ya utiaji wa saini ya mkataba wa mradi wa ujenzi wa daraja hilo kati ya Tanroad na Sumitomo.

"Kama ilivyo kawaida Tanroad itahakikisha mkandarasi huyo na mhandisi mshauri msimamizi wanafanya kazi yao kwa uweledi wa hali ya juu. Tunataka kazi ikamilike ndani ya muda, kwa viwango na gharama zilizokubalika," amesema Mfugale.

Amesema wamekubaliana na Sumitomo kujenga daraja hilo kwa Sh22.42 bilioni kwa muda wa miaka miwili wakati usimamizi wa mradi huo utafanywa na kampuni ya Ingerosec Corporation ya Japan kwa Sh2.86 bilioni na kufanya gharama kufikia Sh25.28 bilioni.

Mwakilishi mkuu mkazi wa Shirika la Maendeleo la Japan (Jica), Toshio Nagase amewataka Watanzania kuiamini kampuni hiyo kwa kuwa ina wahandisi makini na watafanya kazi kama ile ya daraja la Mfugale.

Kwa upande wake, waziri wa ujenzi, uchukuzi na mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema hatua hiyo inaonyesha ushirikiano bora kati ya Tanzania na mataifa ya nje  na kwamba daraja hilo litapunguza foleni jijini Dar es Salaam.