Mchezo ulivyochezeka hadi kukamatwa kwa dhahabu ya mabilioni

Muktasari:

Watu watatu walikamatwa Januari 4, mwaka huu wakiwa na shehena hiyo mithili ya matofali sambamba na gari aina ya Toyota Kruger likiwa na begi lililokuwa na kiasi hicho cha fedha.

Siku chache baada ya tukio la kukamatwa kwa kilo 323.6 za dhahabu na fedha taslim Sh305 milioni zikisafirishwa kutoka Mwanza kwenda mkoani Geita na baadaye askari waliokuwa wakifuatilia mzigo huo kuhojiwa, Rais John Magufuli ameeleza namna mchezo huo ulivyochezeka.

Watu watatu walikamatwa Januari 4, mwaka huu wakiwa na shehena hiyo mithili ya matofali sambamba na gari aina ya Toyota Kruger likiwa na begi lililokuwa na kiasi hicho cha fedha.

Bila kuwataja majina, Rais Magufuli ameeleza namna polisi hao walivyongia katika sakata hilo na kuwa sehemu ya wanaochunguzwa kuhusiana na uhalifu huo uliokuwa na lengo la kuhujumu uchumi.

Akielezea sakata hilo wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi wapya aliowateua akiwemo Waziri wa Madini, Doto Biteko, Rais Magufuli alimpongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kwa kufanikisha kukamatwa watuhumiwa na polisi hao.

“Nimefurahishwa na jinsi ulivyolishughulikia lile suala la madini kule Mwanza, IGP umefanya kazi nzuri hasa ya kuwashika polisi waliokuwa wanachukua rushwa.

“Unajua hii ‘ishu’ watu hawaijui, nimesoma gazeti moja linasema wale polisi waliohusika kushika wamewekwa ndani, nani amesema walihusika kushika. Sasa watu wa magazeti muwe mnajifunza kuuliza vizuri ‘information’ (taarifa).

Aliendelea “Kwa taarifa nilizonazo wale watu (wahusika wa madini) walishikwa Misungwi, Mwanza tarehe 4, wakarudishwa mjini. Walikamatwa na askari nane wakiongozwa na Superintendent wa polisi. Walipoona wamewashika na mali ile wakawapekeka kituo cha polisi, lakini hawakuingia ndani walibaki na mtuhumiwa kwenye gari wakijadiliana kiasi cha kuwapatia”.

Alieleza ana taarifa kwamba askari hao waliahidiwa Sh1 bilioni na usiku waliondoka kituoni hapo bila ya kutoa taarifa kwa mtu yeyote.

“Hata Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) hakuwa anafahamu chochote na kuna taarifa kuna fedha tayari walishapewa za hongo. Walipewa kwanza Sh400 milioni kisha Sh300 milioni wakaondoka, wakaenda kwenye kivuko wakiwa nao.

“Kivuko kikatoka hadi Kamanga wakiwa nao wanasubiri hizo Sh300 milioni zilizobaki. Yule aliyekuwa ameshikwa aliwaambia kuwa hizo zilizosalia wataenda kuzipata Sengerema, hivyo wakawa wanaenda naye wakimsindikiza kwa gari la polisi, mafuta ya Serikali.

“Walipokuwa wanawasindikiza ndipo taarifa nyingine zikatoka na kuwafikia mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella na mkuu wa wilaya ya Sengerema na mimi nikaongea nao nikawaambia lazima muwashike hao wanaokuja.

“Walipofika pale Sengerema wakakuta road block (kizuizi) wakashikwa. Waliposhikwa (watuhumiwa na yule aliyekuwa akipeleka fedha) hawa polisi wakapiga king’ora wakidai walikuwa wanawafuatilia,’’ alisema kuhusu sakata la dhahabu hiyo inayotajwa kuwa ya mabilioni.

“Ulipokuwa nao kwenye gari, usiku kucha hadi ukasafiri nao kwenye kivuko hukupiga king’ora walipofika Sengerema baada ya kuona polisi wengine wanawafuatilia ndipo walipojidai kupiga king’ora, ila wakakamatwa” alisema.

Rais Magufuli alisema hatua hiyo ilimfanya kutoa maelekezo kwa mkuu wa mkoa kwamba askari hao wanyang’anywe silaha, wapigwe pingu na warudishwe Mwanza. “Sasa wanahojiwa kisha watapelekwa kwenye mahakama ya kijeshi, itategemea watakavyokuwa wanajibu na baadaye watapelekwa kwenye mahakama ya kitaifa (kiraia),”” alisema.

Rais Magufuli alimsifu IGP Sirro kuwa alisimamia vizuri suala hilo kwani licha ya kufahamu kuwa waliofanya hivyo ni askari wake, lakini aliwachukulia hatua kwa kuwa wameliaibisha jeshi la polisi.

“Jeshi la polisi linafanya kazi nzuri na polisi wengi ni waaminifu, lakini kama ilivyo kibinadamu wapo wachache waharibifu na ndiyo maana nampongeza IGP alisimama kikamilifu katika hili maana ungekaa kimya na jinsi nilivyokuwa nalifahamu ningekuhusisha katika hili, lakini umefanya vizuri nakupongeza tena huyo Superintendent wa Polisi aliyekuwa akisindikiza huo mzigo nimepata taarifa umemvua vyeo maana amelitia aibu jeshi,” alisema.

Kuhusu madini, Rais alimuagiza Biteko kuanza na uanzishaji wa vituo vya madini vitakavyokuwa na jukumu la kuratibu dhahabu.

Katika hilo pia alimwelekeza Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Florens Luoga kuwezesha uanzishwaji wa vituo hivyo na kushiriki kwenye biashara ya madini kwa kununua kutoka kwa wachimbaji wadogo.

“Hivyo vituo ndio vitakuwa daftari letu kujua ni kiasi gani cha dhahabu kinauzwa nje. Wanaouza nje wawe kwenye rekodi, bora tuwe na dhahabu nyingi tumeihifadhi pale benki kuu itatusaidia hata uchumi ukiyumba.

“Tume ya madini ikafanye kazi sio kuishia kutoa leseni tu, mpaka siku moja nijichague mwenyewe kuwa waziri wa madini,” alisema.

Alisema changamoto zilizopo kwenye sekta hiyo zinatokana na uongozi wa wizara hiyo kushindwa kuwajibika ipasavyo hali inayosababisha nchi kukosa fedha nyingi zinazotokana na madini.

“Sekta ya madini bado ina changamoto kubwa sana, ripoti inaonyesha nchi inayoongoza kwa kuuza dhahabu Afrika Mashariki si Tanzania wakati nchi yetu ndiyo inaongoza kuwa na dhahabu nyingi! Lazima tujiulize ni wapi tunakosea.

“Kuna udhaifu ambao wizara ya madini haiwezi kuukwepa. Kama tuna sheria nzuri, maeneo mengi ya kuchimba dhahabu je tumewahi kujiuliza wanapochimba wanauza wapi na wanapouza tunapata mapato asilimia ngapi.

“Kwenye sheria kuna maelekezo ya kuanzishwa vituo vya madini, je viko vingapi? Hivi vingesaidia kujua kiwango cha madini kinachopatikana na kinauzwa wapi. Inauma unapoona kilo zaidi ya 300 zenye thamani ya zaidi ya bilioni 30 zinakamatwa zikisafirishwa. Wameshaiona Tanzania ni nchi ambayo unaweza kufanya lolote,” alisema Magufuli.

Mapema wiki hii Waziri Biteko aliliambia Mwananchi kuwa Serikali ina mtandao unaosaidia upatikanaji wa taarifa za utoroshaji wa madini.

“Serikali inawatambua na inawaona kila mahali. Kwa sasa wamebakia wachache... Inasikitisha kuona mchimbaji mdogo analiibia Taifa lake wakati mipango ya Serikali ni kumwezesha mchimbaji wa ndani,” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi Kanda ya Afrika wa Shirika la Kufuatilia Usimamizi wa Rasilimali za Asili (NRGI), Silas Olang alisema changamoto iliyopo ni uadilifu kwa wasimamizi waliopewa dhamana na Serikali.

“Kuna wakaguzi wa migodi wanaopata taarifa za uzalishaji na usafirishaji wa madini, wamechimba kiasi gani, wamepata kiasi gani kwa hiyo hakuna kitu kingine zaidi ya uadilifu kwa wachimbaji na wasimamizi,” alisema.