Mchungaji KKKT amuomba Magufuli kuwaachia watu wazungumze

Muktasari:

  • Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Amani Lyimo amemweleza Rais wa Tanzania, John Magufuli kwamba anahitaji kuwaacha watu wakazungumza siyo kuwabana

Dar es Salaam. Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Amani Lyimo amemuomba Rais wa Tanzania, John Magufuli kuwaachia uhuru wananchi wazungumzie inapowezekana kwa sababu hiyo ndiyo demokrasia.

Mchungaji Lyimo amesema hayo leo Jumatano Januari 23, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam katika kikao kati ya Rais Magufuli na viongozi mbalimbali wa madhehebu ya dini.

Amesema Watanzania wengi wanahofu hata kama haambiwi na watendaji wake ila wengi hawathubutu kuzungumza licha ya kuwa anafanya mambo mengi mazuri.

“Kwa kazi unayoifanya watu hawatachagua maneno bali watachagua kazi, kwa hiyo kama kuna uwezekano waachie pumzi kidogo wazungumze lakini hawatakushinda kwa maneno yao,” amesema Lyimo.

Naye Askofu wa Kanisa la Uzima na Ufufuo, Joseph Gwajima ameomba kuwapo kwa maeneo ya kuabudia ya Wakristu katika sehemu ya kusafiria na maeneo ya kazi kama ilivyokuwa kwa waumini wa dini ya Kiislam.

“Wakristu siyo kwamba tunaabudu Jumapili tu, hapana. Ila wakati wote unahitaji kusali kama ilivyo kwa wenzetu. Mahali pa kuabudia ni watu wote tunahitaji ila yawekwe kwa utaratibu maalumu,” amesema Askofu Gwajima.