Mchungaji Peter Msigwa aanza kampeni za ubunge kiaina

Muktasari:

  • Mbunge Chadema Iringa Mjini, Peter Msigwa amesema hali ya maisha imekuwa ngumu hivyo kama anatokea mtu ama chama wakawaahidi wananchi fedha ili wawachague wachukue lakini kura wapigie chadema. Amesema mwaka 2020 atawania tena nafasi ya ubunge wa jimbo lake kwa mara ya tatu.

Iringa. Mbunge Chadema jimbo la Iringa mjini Peter Msigwa amewaambia wananchi wa  Iringa kuwa atawania nafasi ya ubunge Iringa 2020 kwani wananchi wa Iringa bado wanamuhitaji kutetea maslahi yao.

Msigwa ameeleza hayo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Mkwawa mjini hapo huku akiwataka wananchi kuwa makini na viongozi wanaowarubuni kwa kuwapa fedha ili wachague chama fulani.

Amesema hali ya maisha imekuwa ngumu hivyo kama anatokea mtu ama chama Fulani wakawaahidi wananchi fedha ili wachague chama hicho wachukue lakini kura wapigie chadema.

 

Msigwa amesema kinachotakiwa ni kuwa na mwakilishi anayetetea na kusimamia matumizi sahihi ya kodi za wananchi wake na si kuwa na mwakilishi ambaye ametanguliza fedha mbele kama inavyotokea kwa wengi wanaopita mitaani.

“Mimi ni mbunge ambaye natetea maslahi ya wananchi ninao waongoza kwani tangu nimeingia madarakani nimepigia kelele mambo mengi mbungeni ambayo tayari yametekelezwa, hivyo najiona ni kiongozi ambaye nawiwa kuendelea kuwaongoza wananchi wa jimbo hili,” amesema Msigwa.

Msigwa amewaeleza wananchi kuwa kwa miaka 9 aliyokuwa mbunge ,chama cha mapinduzi hawajawahi kuacha kumtukana katika mikutano ya hadhara jambo ambalo linawachukulia muda chama hicho huku yeye akitumia majukwaa ya mikutano kuwaeleza wananchi amewatendea kitu gani.

Aidha amesema kuwa nia ya yeye kugombea ubunge 2020 ni kwa ajili ya kutetea kodi za wananchi ambazo Serikali inazitumia vibaya katika kujinufaisha na kuwalaghai wananchi kuwa fedha hizo ni zao.

“Hakuna kiongozi anayeweza kujenga barabara kwa fedha yake huo ni uongo bali ni kodi za wananchi ndio zinajenga barabara, mkimsikia kiongozi ,serikali ama chama fulani kinasema kimejenga barabara mjue ni uongo,” amewaambia wananchi.

Kwa upande wake meya wa manispaa ya Iringa Alex Kimbe amesema halmashauri ya Iringa imekuwa bora katika kila sekta ya maendeleo kutokana na halmashauri hiyo kuongozwa na Chadema.

Amesema 2020 wananchi wamchague Msigwa huku wakimuongezea madiwani ili halmashauri ya Iringa iendelee kuongozwa na chadema ili waweze kuwatetea wananchi na kuwaletea maendeleo ikiwemo miradi mbalimbali.

“Tunapoelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa baadaye chagueni wenyeviti wa mitaa kutoka Chadema na kwenye uchaguzi mwakani chagueni madiwani na mbunge kutoka Chadema ili Halmashauri iendelee kuwa chini ya Chadema na kuweza kutetea haki za wanyonge,” amesema.

Mmoja wa wananchi waliokuwepo kwenye mkutano huo James Humbe amesema Msigwa amekuwa mfano wa kuigwa kwa kuwa amekuwa akitoa elimu ya uraia na si kutoa fedha kama ambavyo wengine wamekuwa wakifanya.

Humbe amesema ni kodi za wananchi wanazotoa kupitia kwenye ununuzi wanaofanya ndizo zinaleta maendeleo hivyo halmashauri zinatakiwa kuwa na uongozi imara ili kusimamia matumizi bora ya fedha hizo.