Mchungaji ataka sheria ya mirathi iangaliwe upya

Mchungaji Daniel Moses

Muktasari:

 

  • Sheria ya mirathi iangaliwe upya kwa sababu watoto wa watumishi wanaopoteza maisha wamekuwa wakiachwa kwenye mazingira magumu

Dar es Salaam. Mchungaji Daniel Moses ameiomba Serikali kuangalia upya sheria za mirathi kwa sababu baadhi ya ndugu wamekuwa wakichukua pesa hizo na kuwaacha watoto katika mazingira magumu.

Ameyasema hayo leo Januari 23, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam alipokutana na viongozi wa dini ili kuzungumza pamoja juu ya masuala yanayohusu nchi.

Amesema tofauti na ilivyo matarajio ya watoto hao baada ya kupoteza wazazi wao kuwa watapata pesa hizo ndani ya siku tatu au nne badala yake imekuwa miaka mingi.

“Hapo sasa ndiyo huibuka wajomba, shangazi na ndugu wengine kuchukua pesa hizo na kuwaacha watoto wengine wadogo kabisa wakiwa hawana mwelekeo wa maisha,” amesema Moses.

Ametumia nafasi hiyo pia kumpongeza Rais kutokana na  shughuli anazozifanya hasa katika kupambana na watu wanaotumia vibaya mali za nchi.

“Mi nilifurahi sana siku ambayo ulikuwa ukilazimishwa kusema Tanzania kuna njaa ukakataa na badala yake ukasema chakula kipo cha kutosha, lakini pia nilifurahi kusikia ukisema Tanzania ni nchi tajiri si maskini hii inathibitisha ukomavu wako,” amesema.

“Wakati unaanza urais ulikuwa kijana kijana lakini kutokana na mambo mengi hadi nywele unazikata na bado miaka mingine saba,” amesema Moses.