Mdee ahojiwa kwa saa mbili, anyimwa dhamana

Muktasari:

Mbunge huyo wa Chadema alihojiwa kwa kauli zake zinazodaiwa za kichochezi na RCO wa Kinondoni alikiri kufahamu jambo hilo lakini hajui lolote kuhusu kupewa au kutopewa dhamana


Dar es salaam. Mbunge wa Kawe (Chadema), Halime Mdee anaendelea kushikiliwa na jeshi la polisi baada ya kuhojiwa na kunyimwa dhamana.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Februari 23, Wakili Hekima Mwasipu alisema Mdee ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema, amehojiwa kwa muda wa saa mbili na kunyimwa dhamana.

Amesema Mdee alipokea wito na mkuu wa upelelezi mkoa wa kipolisi Kinondoni (RCO) leo kufika kituoni hapo kwa ajili ya mahojiano kutokana na kauli ya uchochezi aliyoitoa kwenye mkutano kata ya Mikocheni Februari 21.

"Polisi wamemhoji kwa masaa mawili kutokana na kauli aliyoitoa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Mikocheni," amesema wakili Hekima.

Amesema maneno anayotuhumiwa kuyatoa siku hiyo alisema "mtu ananunua ndege badala ya vifaa vya zahanati hii ni akili au matope."

Mdee ambaye alifika kituoni hapo saa tatu asubuhi alianza kuhojiwa saa 6:15 hadi saa 8:20 ambapo baada ya mahojiano hayo alinyimwa dhamana.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kinondoni, Mussa Taibu alisema taarifa za kuitwa kwa Mdee anazo ili suala la kunyimwa dhamana hafahamu na yuko kwenye kikao.

"Aliyekwambia kanyimwa dhamana nani, nafahamu alitakiwa kuripoti, kwa sasa niko kwenye kikao," alisema Kamanda Taibu.