Mdee alivyoponyoka katika mtego kufutiwa dhamana kama Matiko

Muktasari:

  • Mahakama imeridhia Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kendelea na majukumu yake ya kibunge nje ya nchi baada ya mdhamini wake, Faresi Robson kuieleza mahakama kuwa sababu ni kwamba mbunge huyo yuko safarini Burundi

Dar es Salaam. Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee ameponyoka katika mtego uliomtumbukiza mbunge wa Tarime Mjini kupitia chama hicho, Esther Matiko kufutiwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wanakokabiliwa na kesi ya jinai, baada ya kujisalimisha kabla ya kusafiri nje ya nchi.

Novemba 23, Matiko alifutiwa dhamana baada ya kufika mahakamani Novemba 8, kwa ajili ya usikilizwaji wa awali wa kesi hiyo inayomkabili yeye, Mdee na viongozi wakuu wa Chadema akiwemo Mwenyekiti Freeman Mbowe.

Mbowe pia alifutiwa dhamana kwa kutofika mahakamani Novemba Mosi na Novemba 8, kutokana na kusafiri nje ya nchi kwa kile alichoeleza kuwa alikwenda kwenye matibabu, huku mahakama ikisema maelezo yake na ya mdhamini wake yalipingana. Jana pia Mdee hakufika mahakamani kutokana na kuwa safarini nchini Burundi anakoshiriki michezo ya wabunge wanawake wa Afrika Mashariki ambayo Matiko alikuwa amekwenda kuandaa mazingira kabla ya kufutiwa dhamana.

Tofauti na Matiko, Mdee hakufika jana lakini mdhamini wake, Faresi Robson aliieleza mahakama kuwa sababu ni kwamba yuko safarini Burundi na kuwa katibu wa Bunge alimwandikia barua Hakimu Mfawidhi kumuombea ruhusa ya mbunge huyo. Mdhamini huyo pia aliieleza mahakama kuwa mshtakiwa huyo anatarajiwa kurejea nchini Desemba 20.

Upande wa mashtaka kupitia kwa wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi ulieleza kuwa hauna pingamizi kwa kuwa na wao wanayo nakala ya barua.

Akitoa uamuzi, Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri alisema anazo taarifa za mbunge huyo kuwa safarini kwa kuwa pia ana nakala ya barua ya Bunge.

Mbali na Mdee, mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche ambaye pia ni mshtakiwa hakuwepo mahakamani na wakili wao, Peter Kibatala alieleza kuwa mdhamini wake amekwama getini kutokana na ulinzi uliokuwepo mahakamani.

Hata hivyo, mahakama iliridhia mbunge huyo aendelee kumuuguza mkewe ambaye taarifa zake zilikuwa pia zimeufikia upande wa mashtaka.

Washtakiwa wengine ni katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji; naibu makatibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar), mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa na wa Bunda Mjini, Ester Bulaya ambao kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo Februari 16, 2018 katika viwanja vya Buibui wilayani Kinondoni wakati wakihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge wa Jimbo la Kinondoni.