Mei mosi ilivyoadhimishwa mikoa mbalimbali

Thursday May 02 2019
mosi pic

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akihutubia wakati wa maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi Duniani Mei mosi yaliyofanyika kimkoa katika Uwanja wa Uhuru jijini, Dar es Salaam jana. Picha na Anthony Siame

Mikoani. Wakati Rais John Magufuli akisisitiza ahadi yake ya kupandisha mishahara ya wafanyakazi kuwa ataitekeleza kabla ya kumaliza muda wake wa uongozi, mikoa mbalimbali nchini ahadi ‘hewa’ kwa wafanyakazi zimegeuka kilio.

Katika mikoa hiyo ambako kulifanyika sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) jana, wafanyakazi bora katika baadhi ya maeneo waliishia kupewa vyeti tu huku wageni rasmi wakihoji sababu za kutopewa fedha kama walivyoahidiwa.

Kagera

Wilayani Bukoba mkoa wa Kagera, Kaimu Mkurugenzi Manispaa ya Bukoba, Josephat Kyebyera na mwenzake wa halmashauri ya Bukoba, Sima Kyamani waliingia matatani baada ya mkuu wa wilaya ya Karagwe, Godfrey Mheluka kuamuru kuwekwa chini ya ulinzi kwa kutoa zawadi hewa kwa wafanyakazi bora.

Baada ya kutajwa wafanyakazi bora, Mheluka ambaye alikuwa mgeni rasmi akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti alimtaka kaimu mkurugenzi halmashauri ya Bukoba, Siima Kyamani kukabidhi fedha alizotaja.

Hata hivyo, kaimu mkurugenzi huyo alikuwa na vyeti pekee.

Advertisement

Hali hiyo ilimshangaza mkuu huyo wa wilaya na kuhoji kama fedha alizosema kaimu mkurugenzi huyo kuwa zipo ofisini ni nzito kubebeka kuliko vyeti na kuagiza polisi kumuweka chini ya ulinzi.

Pia Kyebyera alijikuta kwenye mshangao baada ya wafanyakazi bora aliowataja kugoma kunyoosha mikono ili kukubali kuwa fedha zao zilikuwa zimeingizwa kwenye akaunti za benki.

Wafanyakazi bora waliotajwa walitakiwa kunyoosha mikono kama maelezo ya kiongozi wao ni kweli na baada ya ya ushahidi kukosekana aliwekwa chini ya ulinzi kwa kutoa zawadi hewa.

Tabora

Sakata kama hilo la Bukoba liliibuka pia Tabora baada ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) mkoani humo kuwachongea wakurugenzi wa halmashauri kuwa baadhi yao hutoa zawadi hewa kwa wafanyakazi bora.

Katika risala yao iliyosomwa na mratibu wa Tucta mkoa, Alex Byangwamu walisema kuna baadhi ya wakurugenzi wamekuwa wakitoa zawadi hewa jambo linalowakatisha tamaa wafanyakazi.

Alisema pia wapo wanaotoa zawadi kidogo na wengine hawatoi kabisa na kwamba baadhi ya wakurugenzi hawajatoa zawadi za 2017 na 2018 hadi sasa.

Akijibu risala ya wafanyakazi hao, mkuu wa mkoa wa Tabora, Agrey Mwanri alimtaka katibu tawala mkoa huo, Msalika Makungu kupelekewa orodha ya waajiri ambao hawajalipa zawadi wafanyakazi wao ili waweze kufikia muafaka.

Hata hivyo, aliwataka waajiri hao watoe zawadi za wafanyakazi wao katika kipindi cha wiki moja kuanzia jana kwa vile ni haki yao.

Mratibu Tucta mkoani humo, Alex Byangwamu alisema maslahi ya wafanyakazi si ya kuridhisha.

“Kwa zaidi ya miaka mitatu sasa watumishi nchini hawajaboreshewa maslahi yao na Serikali imekuwa ikitoa ahadi zisizotekelezeka na kama kuna zinazotekelezwa basi ni chache,” alisema.

Arusha

Jijini Arusha ujumbe wa kutaka nyongeza ya mishahara ulitawala mabango ya wafanyakazi wa Serikali na sekta binafsi.

Wakipita mbele ya Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Idd Kimanta, wafanyakazi walibeba mabango yakiwa na ujumbe mbalimbali kuhusu kupandishwa mishahara.

Baadhi ya wafanyakazi walibeba mabango yaliyoeleza Tanzania ya viwanda lazima iendane na nyongeza ya mishahara.

Manyara

Mkoani Manyara eneo la Mirerani watumishi wa Serikali walitakiwa kuwa na subira kuhusu kupandishwa mishahara, huku ofisa tarafa wa Moipo wilayani Simanjiro, Joseph Mtataiko akieleza matumaini yake kuwa Rais Magufuli atatekeleza suala hilo.

Dar

Katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alimuagiza katibu tawala wa mkoa (Ras) na wakurugenzi wa manispaa kuhakikisha kila mfanyakazi anayestahili kupanda daraja apandishwe kabla mwezi Mei haujaisha.

Aliwataka maofisa utumishi wabadilike vinginevyo watabadilishwa wao. Alisema watumishi hao wamekuwa hawatoi likizo kwa watumishi wanaostahili, jambo ambalo linatengeneza matabaka sehemu za kazi.

“Wenye sifa ndani ya mwezi huu lazima wawe wamepandishwa madaraja. Kwa hiyo Ras na timu yako mjipange kutimiza takwa hili la kisheria,” alisema Makonda na kushangiliwa na watumishi waliohudhuria sherehe hizo.

Awali akizungumza kwenye sherehe hizo, Mwenyekiti wa Tucta mkoa huo, George Faustine alisema changamoto kubwa inayowakabili wafanyakazi ni kutopandishwa madaraja licha ya kuwa na sifa zote.

Baadhi ya wafanyakazi waliohudhuria sherehe hizo waliitaka Serikali kuongeza mishahara na kupandishwa madaraja kwa sababu gharama za maisha zimepanda.

Morogoro

Mkoani Morogoro mkuu wa mkoa huo, Dk Stephen Kebwe aliwataka wafanyakazi kutimiza wajibu wao kwa kufanya kazi kwa bidii, maarifa na uadilifu pamoja na kudumisha umoja, mshikamano na upendo baina yao na waajiri kabla ya kudai haki zao za msingi ikiwamo kuongezewa mishahara.

Akisoma risara kwa niaba ya wafanyakazi wa mkoa huo, katibu wa chama cha wafanyakazi wa sekta ya mawasiliano ya simu Tanzania (Tewuta), Clody Kobelo aliiomba Serikali kuangalia upya mishahara ya watumishi wa umma na binafsi ili kuwapa morali ya kazi.

Dodoma

Mkoani Dodoma, mkuu wa mkoa huo, Dk Binilith Mahenge alionyesha kukerwa na halmashauri pamoja na taasisi ambazo zimekuwa zikitoa ahadi hewa kwa watumishi wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani huku akitoa siku tatu ahadi hizo ziwe zimetekelezwa.

Rukwa

Wilayani Sumbawanga mkoa wa Rukwa Tucta ililalamikia kitendo cha mifuko ya hifadhi ya jamii kuipuuza Serikali na kuendelea kutumia utaratibu wa kikokotoo kipya kinyume cha taratibu.

Mratibu wa Tucta Rukwa, Nashon Kabombwe akisoma risala ya wafanyakazi katika mji mdogo wa Leala wilayani humo alisema inasikitisha sana kuona bado baadhi ya mifuko ya kijamii ikipingana na agizo la Rais Magufuli aliyeagiza kusitishwa kwa matumizi ya kikokotoo kipya hadi ifikapo mwaka 2023.

Mkuu wa mkoa huo, Joachim Wangabo aliagiza taasisi zote za serikali kuanzisha mabaraza wa wafanyakazi ili kusikiliza kero za watumishi sehemu ya kazi na kuzitafutia ufumbuzi.

Kilimanjaro

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira alisema maslahi bora kwa wafanyakazi yanapaswa kuendana na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Akihutubia wafanyakazi katika viwanja vya chuo kikuu cha ushirika mjini Moshi, Mghwira alionyesha kutofurahishwa na utoaji wa huduma katika baadhi ya maeneo, ikiwamo hospitali ya rufaa ya KCMC na hospitali ya rufaa mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi na kuwataka watumishi kubadilika.

Mkuu huyo pia aliwanyooshea kidole walimu, akieleza kuwa ni aibu mtoto kumaliza elimu ya msingi huku akiwa hajui kusoma na kuandika, huku walimu wakiwa wanakwenda kazini kila siku na kudai mshahara na maslahi mazuri.

Awali, akisoma risala ya wafanyakazi, Katibu wa Mkoa wa Chama cha Sekta ya Mawasiliano Tanzania, Francis Kessy alisema baadhi ya halmashauri hazifanyi vikao vya mabaraza ya wafanyakazi kwa mujibu wa sheria, jambo linaloibua maswali juu ya namna bajeti za halmashauri zinapitishwa.

Imeandikwa na Robert Kakwesi (Tabora), Joseph Lyimo (Manyara), Mussa Juma (Arusha), Phinias Bashaya (Bukoba), Peter Elias (Dar), Mussa Mwangoka (Sumbawanga), Nazael Mkiramweri (Dodoma), Hamida Sharif (Morogoro), Florah Temba na Yuvenal Theophil (Moshi).

Advertisement