Meneja tume ya madini mbaroni akituhumiwa kuiba madini

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linamshikilia Dornald  Njonjo (30), meneja wa maabara wa tume ya madini kwa tuhuma za kuiba madini ya dhahabu mali ya Serikali ya Tanzania  yenye thamani ya  Sh507 milioni

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linamshikilia Dornald  Njonjo (30), meneja wa maabara wa tume ya madini kwa tuhuma za kuiba madini ya dhahabu mali ya Serikali ya Tanzania  yenye thamani ya  Sh507 milioni.

Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Julai 11, 2019 na Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam,  Lazaro Mambosasa imeeleza kuwa madini hayo yenye uzito wa kilo 6.244 yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye kasiki katika ofisi za wakala wa madini Masaki, jijini Dar es Salaam

Amesema Juni 29, 2019 polisi walipata taarifa kutoka kwa ofisa madini wa mkoa wa Dar es Salaam, Ally Sadick baada ya kugundua upotevu wa madini hayo yaliyokamatwa  mwaka 2017 bandarini Zanzibar yakisafirishwa  kinyume cha sheria.

Baada ya kupata taarifa hizo polisi walianza uchunguzi mara moja na kubaini kuwa madini hayo yaliibiwa na Njonjo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa baada ya mtuhumiwa kuhojiwa alikiri kuiba kidogo tangu Desemba 2018 na kueleza kuwa aliyauza katika duka la kuuzia vito vya dhahabu huku akifanya mpango wa kuyarudishia kwa kuweka madini bandia.

Katika hatua nyingine jeshi hilo linawashikilia watu saba kwa tuhuma za kuvunja  maduka na kuiba bidhaa mbalimbali pamoja na Bajaji mbili.

Tukio hilo lilitokea Julai 9, 2019 eneo la Ukonga na taarifa ilipokelewa katika kituo cha Polisi Stakishari ambako upelelezi ulifanyika na kufanikisha kukamatwa kwa watu hao siku iliyofuata.

Pia jeshi hilo limekamata  silaha moja aina ya bastola Fatin 13-Turkey  yenye namba T.0622010J00535 ikiwa na risasi tisa.

Silaha hiyo ilikamatwa usiku wa Julai 4, 2019 eneo la Mbezi Tangibovu ambako kikosi maalum cha kuzuia na kupambana na majambazi kilimkuta nayo Michael Stellu.