Mengi asirithiwe mali bali utashi

Muktasari:

  • Mtakatifu Valentine alifanana kwa kiasi kikubwa na Mzee wetu Reginald Mengi ambaye pamoja na kubanwa na shughuli nyingi, hakusita kugawa muda na kipato chake kwa wahitaji. Wengi wanamlilia wakikumbuka fadhila zake kwa jamii bila kujali dini, kabila, itikadi wala nini sijui.

Mnamo mwaka 1999 Lucky Dube aliachia albamu ya “Slave” ikiwa na wimbo wa “The Hand That Giveth”. Wimbo ulijaa maneno ya hekima ukinukuu baadhi ya mistari ya Vitabu Vitakatifu ukisema maneno haya:

“Ni tajiri wa aina gani wewe usiyejali watu masikini wala wasio na msaada? Wenzio wanasoma Kitabu Kitakatifu na kuelewa maneno yasemayo ‘Ubarikiwe mkono utoao zaidi ya mkono utwaao’. Hujisikii hata uchungu?”

Ni maneno machache lakini yaliyobeba uzito usiomithilika hasa kwa watu wanaohusika nayo. Bila shaka aliona jinsi walimwengu wanavyohusudu kumiliki kwa namna yoyote kila wakionacho. Lakini baada ya kumiliki na kujitwalia usambe hawakuangalia kushoto, kuume wala nyuma yao. Vyao walivifanyia choyo wakati vya wenzao wakavitolea udelele.

Vitabu vyote vitakatifu hufagilia tabia ya kujitolea. Mbali na sadaka na zaka kwenye nyumba za ibada, vinasema Yule anayetoa misaada kwa wahitaji wakiwemo masikini, wagonjwa, wajane na mayatima hupata thawabu maradufu.

Mfano mmojawapo wa watu wa aina hii ni Mtakatifu Valentine. Sifa mojawapo iliyompaisha ni kujitolea kuelimisha vijana umuhimu wa maadili ya kibinadamu ikiwemo kufunga ndoa na kujenga familia badala ya kuendekeza ngono.

Pia alijikita kusaidia wahitaji bila kujali uhusiano wake nao. Inasemekana alijipangia ratiba ya kutembelea wagonjwa na kuwapatia misaada midogo midogo kama chakula na dawa.

Mtakatifu Valentine alifanana kwa kiasi kikubwa na Mzee wetu Reginald Mengi ambaye pamoja na kubanwa na shughuli nyingi, hakusita kugawa muda na kipato chake kwa wahitaji. Wengi wanamlilia wakikumbuka fadhila zake kwa jamii bila kujali dini, kabila, itikadi wala nini sijui.

Sifa ya kujitolea si kugawa fedha tu. Ni utashi wa kusaidia mahitaji ya wahitaji ili waweze kujiondoa katika kifungo hicho. Fedha inaweza kutumika ikibidi lakini kuna ukweli kuwa fedha pekee haiwezi kuwa msaada. Wachina wana msemo wao usemao “usinisaidie kwa kunilisha samaki, bali nisaidie kunifundisha kuvua samaki”.

Kwenye msemo huu utaona kuwa mtu akiwa na njaa na kukuomba msaada, ukimpa chakula utakuwa umemsaidia kwa siku hiyo tu. Kesho itamlazimu kuomba tena, na kadhalika kesho kutwa. Lakini ukimfundisha namna ya kutafuta chakula utakuwa umesaidia kutokomeza njaa yake.

Nilianza kuona juhudi za Mzee Mengi tangu miaka ya 90 wakati akifanya jitihada za kuwakwamua vijana kutoka kwenye janga la umasikini. Ikumbukwe kuwa miaka ile kulikuwa na tatizo kubwa la ajira. Vijana wengi waliohitimu masomo hawakuwa na namna ya kujiendeleza.

Pia elimu ya ujasiriamali haikuwapo kabisa nchini. Ni watu wachache waliobahatika kusoma nje ndio tuliona wakifanya shughuli za kujiajiri ukiwemo ujasiriamali. Hawa waliweza kuwaajiri vijana wetu wachache lakini kwa malipo yasiyofanana na kazi wala yasiyokidhi mahitaji ya msingi.

Ndipo Mzee wetu akazindua “Saidia Kuondoa Umasikini kwa Vijana” (Skuvi). Nadhani sijakosea sana urefusho huo. Katika mpango huu makundi ya vijana yalijikusana na kuteua uongozi wao. Wakaorodhesha majina na shughuli za uzalishaji mali ambazo wangefanya pamoja na kuwasilisha michanganuo yao. Wataalamu waliwasaidia kunyoosha mipango na wakapatiwa mikopo na misaada ya kujiendeleza.

Mpaka sasa mazao ya Skuvi yangali yakionekana ingawaje vikundi vingi viligawana mitaji na kila mtu akaanzisha shughuli yake binafsi. Na kama isemwavyo kuwa hata kenge huzamia msafara wa mamba, vijana wengine waligawana na kuinywa mitaji yao mapema. Hawakubugudhiwa maana ilikula kwao kimya kimya.

Sifa ingine ya mtoaji ni kutojigamba. Iliandikwa kuwa utoapo msaada hata jirani yako asisikie. Utoapo kwa mkono wa kuume, wa shoto usione kinachoendelea. Hilo nililipigia mstari siku ya misa ya kumwombea, komredi mmoja alipotaja fedha nyingi sana alizosaidiwa kimya kimya kulipa deni.

Ni wengi wasio idadi waliopata misaada ya aina hiyo. Lakini hiyo siyo ishu kubwa kama misaada kwa wenye ulemavu. Hii ndiyo hasa inayowatoa watu machozi hata sasa baada ya kutafakari maana yake halisi.

Walemavu ni watu waliodhalilika tangu enzi na enzi. Pamoja na kampeni zilizokuwa zikiendelea kuwaweka kwenye daraja sawa na binadamu wengine, taasisi ambazo zingeweza kuwabeba zilikatishwa tamaa na gharama za mahitaji yao. Wenye watoto walemavu wanaelewa nina maana gani. Sasa anapotokea mtu wa aina ya Mzee wetu anafanana kabisa na malaika kwao. Kwanza anawarudishia utu wao kwa jinsi anavyowathamini. Kisha kwa vipawa alivyojaliwa na Mwenyezi Mungu anawatengenezea wepesi kielimu na kimaisha. Mtu hataishi kwa mkate pekee…

Hivyo ni juu yetu baada ya kutafakari hayo, kujiweka kwenye nafasi ya kumrithi mzee wetu. Msianze kukenua meno mkidhani kumrithi utajiri, hapana. Tumrithi kujitoa kwa wahitaji. Hakika hiyo ndiyo namna pekee ya kumuenzi na kupata baraka.