Mengi awatangazia neema wenye ulemavu

Muktasari:

  • Mengi amewaambia walemavu kuwa wanaweza kuwa matajiri kumzidi yeye na kwamba ulemavu si umaskini kwa kuwa wanaweza na watafanikiwa.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi amesema anatarajia kufungua kiwanda cha kutengeneza simu za mkononi 'smart phone' Machi mwaka 2019 na kuajiri watu wenye ulemavu.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi viungo bandia kwa walemavu zaidi ya 120 vinavyotolewa na kampuni ya Camal Group ya jijini Dar es Salaam, Mengi amesema ajira hiyo ni ahadi yake aliyoitoa ili  kuwasaidia watu wenye ulemavu.

Amesema ulemavu si umaskini na kosa pekee wanaloweza kufanya kwenye maisha yao ni kusema 'siwezi'.

"Nafurahi kujumuika na walemavu napata raha sana, ulemavu sio umaskini, kupoteza mguu sio mwisho wa dunia unaweza tumia kilichopo ukafanya maajabu," amesema Mengi.

Amewataka walemavu kutokata tamaa badala yake waone wanaweza kufanikiwa kimaisha na kuwa matajiri wakubwa.

Kupitia taasisi yake ya watu wenye ulemavu, Mengi ametoka Sh200,000 kwa kila mlemavu aliyepata kiungo bandia kama mtaji wa biashara au kuendeleza kipaji chake.

Naye Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Stella Ikupa amewataka watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa ya ajira kutoka kwenye kiwanda kitakachozinduliwa na Mengi.

"Aliahidi kiwanda hiki, niwaombe tu ndugu zangu muwe wajanja na kuchangamkia fursa hii," amesema Ikupa.

Tayari zaidi ya walemavu 120 wamekabidhiwa viungo bandia na Taasisi ya Camal Group ili kurejesha furaha yao.