Mengi kuzikwa kando ya mwanae, wazazi wake -VIDEO

Muktasari:

  • Shughuli ya kuchimba kaburi la kumhifadhi aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi imeanza leo Jumatatu Mei 6, 2019 kijijini kwake Nkuu, Machame mkoani Kilimanjaro. Kaburi hilo linachimbwa kando ya makaburi ya wazazi wake, mwanae

Hai. Shughuli za uchimbaji kaburi atakalozikwa aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi imeanza leo asubuhi Jumatatu Mei 6, 2019 nyumbani kwake Kijiji cha Nkuu Sinde Machame Mashariki, mkoani Kilimanjaro.

Mwananchi Digital imefika nyumbani hapo na kushuhudia vijana wakichimba kaburi eneo ambalo walikozikwa wazazi wake na mwanae, Roodney Mengi aliyefariki mwaka 2005.

Mfanyabiashara huyo maarufu ndani na nje ya Tanzania alifariki dunia usiku wa kuamkia Alhamisi   Mei 2, 2019 akiwa Dubai, Falme za Kairabu alikokuwa akipatiwa matibabu.

Mwili wa Mengi unatarajia kuwasili leo Jumatatu saa 9:00 alasiri katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam (JNIA), kisha utapitishwa barabara mbalimbali hadi Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo.

Kesho mwili huo utaagwa katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, baadaye utapelekwa nyumbani kwake Kinondoni utakapolala hadi Jumatato asubuhi utakaposafirishwa kwenda Machame kwa mazishi yatakayofanyika Alhamisi hii  Mei 9, 2019.