Meya wa Chadema ajiuzulu, atangaza kuhamia CCM

Muktasari:

Leo Jumamosi, Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko ambaye pia ni diwani wa Bonyokwa (Chadema) ametangaza kujiuzulu nyadhifa zote na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM)

Dar es Salaam. Meya wa Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam, Charles Kuyeko (Chadema)  leo Jumamosi Machi 23, 2019 ametangaza kujiuzulu uanachama wa Chadema na kujiunga na CCM.

Kuyeko ambaye ni diwani wa Bonyokwa amesema anamshukuru Rais wa Tanzania, John Magufuli ‘Kwa kazi ya ajabu ya kutukuka’ ambayo anaifanya na kuomba Watanzania kumuunga mkono.

“Niwashukuru Chadema ambao walinipa nafasi ya kugombea kupitia kwao na mimi sikuwadharau, nitaendelea kuwaheshimu lakini mapenzi yangu ya dhati ni CCM,” amesema Kuyeko.

Amesema alikuwa akifurahishwa na jinsi Rais Magufuli akiwa Waziri wa Ujenzi jinsi alivyofanya kazi.

Mwananchi limezungumza na Mkurugenzi wa Ilala, Jumanne Shauria kuhusu taarifa hizo ambapo amesema yuko nje ya ofisi lakini akadokeza, “Nimesikia taarifa hizo lakini sijapata barua.”

Naibu Meya wa halmashauri hiyo, Omary Kumbilamoto amesema, "Ni kweli babu (Kuyeko) amejiuzulu leo.”

"Kwa sasa mimi ndiye ninakaimu baada ya yeye kujiuzulu wadhifa huo," amesema Kumbilamoto ambaye aliwahi kuwa diwani wa CUF kabla ya kujiuzulu na kujiunga na CCM mwaka 2018.

Msemaji wa Chadema, Tumain Makene amesema na wao wanaona taarifa katika mitandao lakini kama chama hawajapata taarifa kamili ya meya wao kujiuzulu na kutimkia CCM.

Hatua ya Kuyeko kutimkia CCM inawafanya Chadema kubaki na mameya wawili katika Jiji la Dar es Salaam ambao ni Boniface Jacob wa Ubungo na Isaya Mwita wa Jiji la Dar es Salaam.

Endelea kufuatilia Mwananchi kupata undani wa habari hii