Mfanyabiashara Tandika ashangaa kudaiwa kodi baada ya kufunga biashara

Ofisa kodi mwandamizi kutoka wilaya ya Temeke. Bakari Mlandula mwenye shati la drafti alifafanua jambo kwa baadhi ya wafanyabiashara waliohudhuria katika hema ya kutoa elimu kwa mlipakodi katika eneo la Tandika

Muktasari:

Wafanyabiashara wameombwa kutoa taarifa za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wanapofunga biashara zao ili kuepuka usumbufu wa kudaiwa malimbikizo ya kodi


Dar es Salaam. Mfanyabiashara wa soko la Tandika, Tatu Ally, amesema elimu ya mlipa kodi inayotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewafikia kwa kuchelewa kwa maelezo kuwa hawajui kama mtu akifunga biashara anaendelea kudaiwa kodi na mamlaka hiyo.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Mei 16, 2019 alipokutwa na Mwananchi Digital katika soko hilo ambalo ni miongoni mwa maeneo yanayotumiwa na TRA kutoa elimu hiyo jijini Dar es Salaam.

Tatu amesema wakati mwingine kutokana na uchumi kutokuwa mazuri watu huamua kufunga biashara bila kutoa taarifa TRA, huku akikiri kuwa miongoni mwa watu wasiofahamu jambo hilo.

“Nashangaa kusikia kuwa ukiwa na namba ya mlipa kodi unaendelea kuhesabiwa na muda wa kulipa kodi unapofika unatakiwa kuiwasilisha sasa nitaleta nini wakati biashara haiendelei na mimi sina hela,” amesema Tatu.

Akijibu suala hilo, Ofisa Kodi Mwandamizi wa TRA Wilaya ya Temeke, Bakari Mlandula amesema ni ngumu   kufahamu kama biashara ya mtu husika haiendelei mpaka atoe taarifa ya kufunga biashara, hiyo ndio njia sahihi anayopaswa kufanya.

“Unapofungua biashara yako kuna asilimia ya Serikali, ukifunga na haujatujulisha tukija kudai kodi uniambie ulifunga sitakuelewa.

 “Badala yake unachoweza kufanya ili tuipokee taarifa ikiwa imechelewa kuwa ulifunga biashara, labda tangu mwaka jana unatakiwa utuletee uthibitisho wa barua ya serikali za mitaa kwa sababu ndio Serikali tunayoiamini,” amesema Mlandula.

Amesema kupitia barua hiyo wanatakiwa kuandikia kuwa kweli mfanyabiashara alipata tatizo akafunga biashara au kama amepata fedha amefungua upya kisha TRA wataipisha hiyo barua.

Pia, aliwakumbusha wafanyabiashara hao kufanya makadirio ya kodi kila baada ya miezi mitatu na kulipa kodi zao kuepuka usumbufu.