Mfanyabiashara kortin kwa kusafirisha dhahabu kinyume cha sheria

Thursday June 20 2019

madini  dhahabu,Mirajdin Tajdin,Mfanyabiashara kortin

Mshtakiwa wa kesi ya kusafirisha madini ya dhahabu bila ya kuwa na kibali, Mirajdin Tajdin (katikati) akiwa katika mahakama ya hakimu mkazi kisutu jijini Dar es Salaam leo. Picha na Ericky Boniphace 

By Hadija Jumanne, Mwananchi. [email protected]

Dar es Salaam. Mfanyabiashara nchini Tanzania, Mirajdin Tajdin(32), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam akikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la  kusafirisha dhahabu bila kuwa na kibali.

Tajdin ambaye ni mkazi wa Mtoni  Mtongani amefikishwa mahakamani hapo leo Alhamisi, Juni 20, 2019 na kusomewa mashtaka na wakili wa Serikali Ester Martin.

Martine amedai mshtakiwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 50/ 2019.

Akimsomea hati ya mashtaka, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Janeth Mtega, Wakili Martin amedai mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo April 30, 2019 katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere( JNIA) uliopo  wilaya ya Ilala.

Amedai siku hiyo ya tukio, mshtakiwa  alikutwa na vipande vya dhahabu vyenye uzito wa gramu 98, vikiwa na thamani ya dola za Marekani 3636.92, sawa na Sh 8, 364,914 Mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika shtaka la  pili, muda na eneo hilo, Tajdin anadaiwa kusafirisha dhahabu hiyo bila kuwa na kibali kutoka Mamlaka husika.

Advertisement

Martin, amedai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba Mkurugenzi wa Mashtaka nchini amewasilisha hati ya kuruhusu Mahakama ya Kisutu kutoa dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo.

Hata hivyo, mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yanayomkabili, alikiri kutenda makosa hayo.

Hakimu Mtega baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashtaka, alitoa masharti ya dhamana kwa mshtakiwa huyo ambayo ni kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua kutoka Serikali ya Mtaa, atakayesaini bondi ya Sh8 milioni.

Mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na kurudishwa mahabusu.

Hakimu Mtega ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 4, 2019  kwa ajili mshtakiwa kusomewa hoja za awali(PH).


Advertisement