Mfuko kulinda mtikisiko bei ya mazao Tanzania mbioni kuanzishwa

Muktasari:

  •  Naibu waziri wa Kilimo wa Tanzania, Hussein Bashe amesema kuanzia kesho Jumatatu Agosti 5, 2019, benki zitaanza kutoa fedha kwa ajili ya kununua pamba kutoka kwa wakulima na Amcos.

Mwanza. Naibu Waziri wa Kilimo wa Serikali ya Tanzania, Hussein Bashe amesema wameanza kupitia sera ya kilimo na wataanzisha mfuko utakaokuwa unalinda mtikisiko wa bei za mazao duniani.

Bashe amesema hayo jana Jumamosi Agosti 3 alipokuwa akifungua y ya nane Nanane jijini Mwanza yaliyohusisha Mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera.

Amesema kama nchi haina uwezo wa kudhibiti bei katika soko la dunia, huenda zao la Pamba lingenunuliwa hata kwa bei ya Sh700, Sh600 au Sh500.

“Nataka nitumie nafasi hii kuwaambia Watanzania, Waziri Mkuu amehakikisha tatizo la pamba iliyojaa mikononi mwa wakulima na Amcos, Jumatatu benki zitaanza kutoa fedha kwa ajili ya kununuliwa,” amesema Bashe.

Amesema mchakato huo wa benki kutoa fedha kwa ajili ya kununua pamba ulikamilika jana usiku Agosti 2 na kikao kilifanyikia Mkoa wa Mwanza katika ukumbi wa Benki ya Tanzania.

Amewataka Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya waondoe vikwazo na wafuate agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la pamba kusafirishwa hadi usiku.

"Muondoe vikwazo kwa kuwazuia wasafirishaji wasisafirishe pamba usiku na katika kipindi hiki cha mwezi mmoja, niwaombe watu wa halmashauri, Wakuu wa Wilaya na Mikoa, agizo hili la Serikali litekelezwe,” amesema Bashe.

Amesema baada ya kupitisha sera na sheria mpya ya kilimo, utaanzishwa mfuko utakao kuwa unakusanya fedha kwa ajili ya kuangalia kipindi ambacho bei ya mazao zimeshuka Serikali iweze kumfidia mkulima asipate hasara kama tatizo lililojitokeza kwenye zao la korosho, pamba na kahawa.