Mfumo mpya wa Huawei utakavyokuwa

Beijing. Mvutano wa Marekani na China umeibua jambo jipya baada ya kampuni ya Huawei ya China kubuni mfumo mpya waa kuboresha simu za mkononi na vifaa vingine ili kushindana na mfumo wa Android wa Marekani.

Mfumo huo wa Huawei -HarmonyOS unaolenga kupunguza utegemezi wake kwa kampuni za Marekani, utakuwa tayari kuwekwa katika skrini za simu, televisheni, saa na magari baadaye mwaka huu.

Mkurugenzi mkuu wa wa kitengo cha walaji cha Huawei, Richard Yu, katika kipindi cha miaka mitatu ijayo itaangalia jinsi ya kuweka mfumo wa HarmonyOS kwenye vifaa zaidi.

Ingawa hakutoa ushahidi, Yu alisema HarmonyOS ni "yenye nguvu zaidi na bora zaidi ya mfumo Android." "Inaweza kuwekwa katika smartphones, bila shaka."

"Mfumo wa HarmonyOS unaweza kuwekwa katika hali ya kuwa na maingiliano na kifaa kingine chochote," ilieleza taarifa ya kampuni hiyo.

Kampuni ya Huawei inasema kuwa imeazimia kuendelea kutumia Android, lakini HarmonyOS utatumika kama mpango mbadala kama mambo yataenda kombo. "Tutaupa kipaumbele mfumo wa Android kwa smartphones, lakini kama hatutatumia Android, tutaweza kuweka mfumo wa HarmonyOS haraka," Yu alinukuliwa a BBC.

Kuwepo kwa mfumo wa simu za mkononi ambao ni chanzo cha wazi, utakuwa ni kwa ajili ya China pekee kwa sasa, ingawa kampuni ina mipango ya kuuleta katika masoko ya kimataifa baadaye.

Tangazo hilo la Huawei limekuja miezi kadhaa baada ya serikali ya Marekani kuweka masharti ya kibiashara nchini Marekani yanayoilenga kampuni hiyo pamoja na kampuni nyingine washirika .

Serikali ya Marekani imeishutumu Huawei kwa kuiba siri za kibiashara na ikasema inaleta hatari kwa usalama wa taifa.

Huawei inapinga shutuma zote hizi na imeamua kuchukua mbinu za kisheria kukabiliana na shutuma za Marekani.