Mgebuka anayetema maji awa kivutio Kigoma

Thursday March 14 2019

 

By Anthony Kayanda, Mwananchi. [email protected]

Kigoma. Baadhi ya wakazi wa Kigoma Ujiji wamejikuta wakisafiri kutoka mitaa wanayoishi na kwenda kutazama samaki aina ya mgebuka anayetema maji baada ya kuzinduliwa leo Alhamisi Machi 14, 2019.

Sanamu hiyo imejengwa eneo la Mwanga sokoni katika mzunguko wa barabara ya Kigoma, Ujiji na Mwandiga.

Mkazi wa Katubuka, Salumu Juma ameiambia Mwananchi baada ya kupata taarifa juu ya uzinduzi wa sanamu hiyo amelazimika kufika ili kuona namna anavyotema maji.

"Hii sanamu imenivutia sana, ilikuwa nikienda Mwanza najiuliza kwa nini wao wana sanamu ya (samaki aina ya) sato halafu sisi (Kigoma Ujiji) tukose? Hii ilikuwa inanishangaza sana," amesema juma.

Mwavita Abdi wa Mwanga mjini Kigoma amesema sanamu hiyo ni kivutio na haina budi kutunzwa ili iendelee kuwa kivutio.

Meneja wa Wakala wa Barabara za Tanzania (Tanroad) mkoa wa Kigoma, Talas Choma amesema sanamu hiyo imejengwa kwa thamani ya Sh7 milioni.

Tanroad wanakusudia kujenga taa kwenye mzunguko huo wa Mwanga sokoni ambapo wanatarajia kutumia zaidi ya Sh100 milioni.

Advertisement