Mgombea wa CCM Arumeru Mashariki apita bila kupingwa

Mgombea ubunge wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki  kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), John Pallagyo

Muktasari:

  • Ametangazwa leo na mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru baada ya wapinzani wake kushindwa kutimiza vigezo

Arumeru. Mgombea ubunge wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki  kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), John Pallagyo amepita bila kupigwa katika nafasi hiyo  baada ya wagombea wenzake 10 kushindwa kukidhi vigezo. 

Msimamizi wa uchaguzi Jimbo hilo, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Meru, Emmanuel Mkongo amesema hayo Leo Ijumaa Aprili 19, 2019 wakati akitangaza matokeo baada ya upitiaji wa fomu zilizowasilishwa .

Mkongo amesema jumla ya wagombea 11 walichukua fomu na kati yao, watatu hawakurudisha na saba fomu zao zimebainika kutokidhi vigezo.

Amesema wapo ambao hawajalipa fedha ya dhamana ya kugombea ubunge  ya Sh50,000, kukosa wadhamini na kurejesha fomu ya kiapo kutoka kwa mwanasheria na hakimu.

Akizungumza baada ya mkurugenzi kumtangaza kuwa kapita bila kupingwa, pallagyo,  amekishukuru chama chake kwa kumuamini na amesema atahakikisha anafuata  nyayo za Rais John Magufuli katika utendaji kazi.

“Pia nitamkumbusha Rais ahadi yake aliyoitoa ya ujenzi wa barabara ya kilometa tano za lami jimboni humo na nitahakikisha jimbo hilo linakuwa la mfano ndani ya muda mfupi,” amesema.

Naye Mmoja wa wagombea kutoka chama cha Demokrasia Makini, Saimon Ngilisho ameunga mkono uamuzi huo huku akikiri kukosa wadhamini kutokana na wananchi kukatishwa tamaa na wapinzani kujiuzulu kabla ya muda wao kufika, hivyo kusababisha kukosa sifa za kugombea.