Mgomo wa daladala Moshi kama kawaida, abiria wasota

Muktasari:

  • Madereva wa magari yanayotoa huduma katika maeneo kadhaa ndani ya mji wa Moshi, wameendelea na mgomo kwa siku ya pili leo, wakipinga kukamatwa na polisi na kudaiwa ushuru wa maegesho.

Moshi. Mgomo wa daladala zinazotoa huduma katika maeneo ya KCMC, Majengo, Soweto na Bonite, manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro umechukua siku ya pili huku madereva wakieleza hawatarudi barabarani hadi magari yaliyokamatwa yatakapoachiwa.

Kutokana na mgomo huo, hali ya usafiri imekuwa ngumu kwa watuamiaji usafiri huo kulazimika kutafuta njia mbadala kuhakikisha wanafika wanakokwenda ikiwamo kwa gharama kubwa zaidi.

Jana Jumatano Machi 13, 2019 magari hayo yalianza mgomo kwa madai ya kupinga kukamatwa na jeshi la polisi kutokana na kugoma kulipa ushuru wa maegesho ya magari wa Sh1,000 kwa siku kuanzia Novemba 19, 2018.

Akizungumza leo Alhamisi Machi 14, 2019 Alfan Shaban ambaye ni dereva wa KCMC, amesema hawataweza kufanya kazi hadi magari yaliyokamatwa na polisi jana yatakapoachiliwa.

“Jana zilikamatwa gari zaidi ya saba na polisi, kwa madai ya kutolipa ushuru na sisi hatuwezi kufanya kazi hadi  yatakapoachiwa na sisi kuhakikishiwa kufanya kazi bila kukamatwa, maana kinachoendelea ni uonevu kwetu,” amesema Shaban.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Michael Mwandezi amesema mgomo huo unatokana na madereva kugoma kulipa ushuru kama sheria inavyoelekeza na hawataweza kuwafumbia macho wale wanaovunja sheria.

Mwandezi alisema kama madereva hao hawataki kulipa ushuru ni vyema wakakaa nyumbani kwa kuwa wale wote watakaoingia barabarani bia kulipa ushuru, wataendelea kukamatwa ili kuhakikisha wanatekeleza sheria.

“Dereva akiwa barabarani ni lazima alipe ushuru, sasa kama hataki akae nyumbani hakuna mtu ambaye atamsumbua, lakini kwa wale ambao wataingia barabarani na hawajalipa ushuru, tutawakamata,” amesema Mwandezi.

 

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachojiri