Mgomo wa daladala Moshi ngoma nzito

Muktasari:

Mgomo wa daladala uliotokana na Bajaj kupakia abiria katika vituo vya mabasi umesababisha adha kwa wakazi wa Moshi, kulazimika kutembea kwa miguu na kukodi bodaboda

Moshi. Mgomo wa daladala mjini Moshi leo Jumatatu Desemba 3, 2018 umesababisha baadhi ya wananchi kutumia pikipiki za kukodi na wengine kutembea kwa miguu kuelekea maeneo mbalimbali.

Mwananchi liliwashuhudia wananchi wao wakitembea kwa miguu huku daladala nyingi zikiwa zimeegeshwa bila kupakia abiria.

Mgomo huo ambao hadi leo saa 7 mchana ulikuwa haujamalizika unatokana na madereva wa daladala kupinga Bajaj kupakia abiria katika vituo vya mabasi.

Wakizungumzia  mgomo huo, madereva wa daladala wamesema mgogoro kati yao na wenye Bajaj ni wa tangu 2013 lakini viongozi wameshindwa kuutatua.

Jackson Kinyaiya  amesema: “Bajaj zinaingia katika maeneo yetu ya biashara na kupakia abiria. Mgogoro huu tumeupeleka katika ngazi mbalimbali lakini hakuna ufumbuzi. Tumeamua kugoma leo ili muafaka upatikane.”

Dereva mwingine wa daladala, Sanael Mushi ameungana na Kinyaiya na kubainisha kuwa baadhi ya viongozi wana maslahi na jambo hilo na ndio sababu wanashindwa kulimaliza.

Kwa upande wake, Hussein Ally amesema haoni faida ya kazi wanayoifanya kwa kuwa imeingiliwa na Bajaj, hivyo ameamua kurejesha funguo za daladala kwa mwajiri wake kwa kuwa hakuna anachokipata.

Akizungumzia sababu za mgomo huo ofisa mfawidhi Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) mkoani Kilimanjaro,  John Makwale amesema chanzo ni  Bajaji kutozingatia sheria na kufanya kazi za daladala.

Amesema kila dereva anatakiwa kutoa huduma kwa mujibu wa leseni yake la sivyo sheria itachukua mkondo wake.

"Maelekezo ambayo tumeyatoa leo tumewataka watu wa Bajaji na daladala watoe huduma kwa mujibu wa leseni zao. Sisi tutaendelea kusimamia sheria na atakayeenda kinyume  tutamchukulia hatua. Bajaj wasiingilie maeneo ya daladala,” amesema Makwale.

Mratibu wa Bajaji  Mkoa wa Kilimanjaro, Rashid Omary amewataka madereva wa Bajaj kufuata sheria na kila mtu kukaa eneo lake kutokana na leseni yake inavyomtaka.