Mgomo wa madereva wa mabasi watua bungeni, Dk Tulia atoa agizo kwa Serikali

Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga akitoa hoja ya kuahirisha bunge ili kujadili mgomo baridi wa madereva wa mabasi nchini, bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

  • Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga ametoa hoja ya kuahirisha shughuli za Bunge leo Jumatano akitaka Bunge lijadili mgomo baridi wa madereva wa mabasi unaoendelea nchini. Naibu Spika, Dk Tulia Ackson ameiagiza Serikali kulishughulikia suala hilo kwa kukutana na madareva na wamiliki wa mabasi

Dodoma. Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinmga leo Jumatano Mei 15  ametoa hoja ya kuahirisha shughuli za Bunge ili kujadili mgomo baridi wa madereva wa mabasi unaoendelea maeneo mbalimbali nchini.

Mlinga akitumia kanuni ya 47 za Bunge amesema: “Hivi ninavyoongea kuna mgomo baridi wa mabasi nchi nzima kuanzia Morogoro madereva wanataka kugoma.”

Amesema madereva hao wanataka kugoma kwa sababu mabasi yamefungwa vifaa maalum vya kudhibiti mwendo ambapo wamekuwa wakipigwa faini na kuchelewesha safari akitolea mfano kama dereva atafuata utaratibu safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro itamchukua saa sita.

Mlinga amesema pamoja na kuchelewesha safari lakini madereva wamekuwa wakipigwa faini zaidi ya Sh 5 milioni katika safari moja jambo ambalo amedia lina viashiria vya rushwa na ucheleweshaji wa safari.

Mara baada ya kutoa maelezo hayuo, wabunge wengi walisimama kumuunga mkono Mlinga.Hata hivyo, Naibu Spika, Dk Tulia Ackson amesema jambo hilo linaweza kushughulikiwa katika utaratibu wa kawaida.

“Serikali ichukue hatua kuona ni mambo gani yanalalamikiwa na madereva, watu wanataka kusafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine na wakati huo huo usalama wao unazingatiwa,” amesema Dk Tulia.

Amesema Serikali ipo bungeni imesikia hoja ya Mlinga ikikutana na madereva na wamiliki wataona ni wapi kunahitaji kushughulikiwa ili kutoathiri wananchi kukosa usafiri.