Mhasibu Arusha adaiwa kutafuna Sh85 milioni kila mwezi

Muktasari:

Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk Maulid Madeni amemtaka mhasibu wa jiji hilo, Charles Jacob kujisalimisha polisi kwa madai ya kutafuna Sh85 milioni za makusanyo ya kila mwezi kuanzia Machi, 2019 katika mizani wa mazao ya chakula.


Arusha. Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Dk Maulid Madeni amemtaka mhasibu wa jiji hilo, Charles Jacob kujisalimisha polisi kwa madai ya kutafuna Sh85 milioni za makusanyo ya kila mwezi kuanzia Machi, 2019 katika mizani wa mazao ya chakula.

Amesema tangu mizani hiyo ilipoanzishwa Machi, 2019 imekuwa ikiingiza Sh3.3 milioni kwa mwezi badala ya Sh88 milioni, kwamba Sh85 milioni kila mwezi hazijulikani zinapokwenda.

Jacob, msimamizi wa mizani hiyo pamoja na wafanyakazi wake wawili,  Thobias Julius na Agness Loishiye wanadaiwa kusababisha upotevu huo wa fedha.

Madeni amewaweka ndani wafanyakazi hao na kuagiza Jacob ambaye hakuwepo kazini kujisalimisha mwenyewe kituo cha polisi kati Mkoa wa Arusha.

Akizungumza leo Jumamosi Julai 20, 2019 Dk Madeni amesema kituo hicho cha kukusanya ushuru hakifanyi vyema na kusababisha fedha nyingi kuishia mikononi mwa wakusanyaji na mhasibu huyo.

“Nilifuatilia muda mrefu ukusanyaji wa mapato nikagundua kuna ulaji mkubwa wa fedha unaofanywa na mhasibu huyo ndio maana leo hajaja hapa.”

“Anaelewa mchezo anaoufanya na wafanyakazi wake nitahakikisha nawaweka ndani wote wanaojaribu kucheza na fedha ya Serikali sitamwonea mtu yeyote huruma,” amesema Dk Madeni

Amebainisha kuwa kuna wafanyakazi wachache wanaiibia Serikali mapato, kuahidi kupambana nao.

Awali, wafanyakazi hao walipewa nafasi ya kujitetea na kubainisha kuwa wameshindwa kukusanya mapato kutokana na magari kuwa machache, hawafahamu kama fedha wanayokusanya kama inafika au haifiki katika halmashauri.

Mchumi wa Jiji la Arusha, Anna Mwambene amesema wamekuwa wakifuatilia vyanzo vya mapato mbalimbali kuangalia utendaji wa kazi, kubaini upotevu wa fedha unaofanywa na watendaji wasio waaminifu.