Miaka 10 Kikoba cha Juhudi care, mtaji wakua mara 5 zaidi

Mwenyekiti wa Kikundi cha Kikoba cha Juhudi Care, Regina Mutanulwa aliyeshika kipaza sauti akiongea na wanachama wakati wakiadhimisha miaka kumi tangu kuazishwa kwa kikoba hicho. Picha na Pamela Chilongola

Muktasari:

  • Kukua kwa mtaji wa kikoba cha Juhudi Care umeweza kuwanufaisha wanachama na kuendeleza mchakato wa kufungua kiwanda cha kusindika karanga.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa kikundi cha Kikoba cha Juhudi Care, Regina Mutainulwa amesema katika kipindi cha miaka 10 mtaji wao umeweza kukua hadi kufikia Sh158 milioni kutoka Sh28 milioni waliyoanza nayo awali.

Mbali na kukua kwa mtaji lakini pia mkakati uliowekwa hivi sasa utawezesha kiwanda cha kusindika karanga kuanzishwa.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka kumi tangu kuanzishwa kwa kikundi hicho chenye wanachama 30 amesema mwaka 2018 walipata faida ya Sh 40 milioni kwa kupitia benki wanakoweka na mikopo wanayokopeshana.

"Utaratibu tulioanzisha mwaka 2017 kuwa kila tunapovunja kikoba mwanachama anaacha Sh800,000 ya faida anayopata tunataka kila mwanachama afikishe Sh10 milioni ili kukuza mtaji wetu zaidi ya Sh158 tuliyonayo sasa."amesema Mutainulwa

Amesema kufanya hivyo pia kutasaidia kuanzisha kiwanda cha usindikaji wa karanga na kuwezesha kununua kununua mashine zenye uwezo mkubwa.

Katibu wa wa kikundi hicho, Margreth Mwankosye amesema kupitia kukopesha kila mwanachama ameweza kunufaika huku akitolea mfano jinsi alivyofanikiwa kufikisha kuku 1000 kutoka kuku 200 aliokuwa akifuga awali.

Naye Mkufunzi wa ujasiriamali kwa vitendo, Elizabeth Kassembo amesema licha ya changamoto ya mtaji lakini wengi wamekuwa wakijitokeza kujifunza utengenezaji keki na mifuko ya mbadala ya karatasi.

"Vijana wakipatiwa ajira haitakuwa tatizo lakini hivi sasa wengi wanajitokeza kujifunza na itawasaidia kuinua kipato chao kwa ujumla,"amesema Kassembo.