Miaka miwili ya ujumbe wa Nape mitandaoni inavyoacha maswali

Muktasari:

  • Takribani miaka miwili sasa mbunge wa Mtama (CCM),  Nape Nnauye amekuwa akitumia ukurasa wa akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter kuzungumzia masuala mbalimbali kwa staili inayoacha maswali

Dar es Salaam. Takribani miaka miwili sasa mbunge wa Mtama (CCM),  Nape Nnauye amekuwa akitumia ukurasa wa akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Twitter kuzungumzia masuala mbalimbali kwa staili inayoacha maswali.

Si ajabu kuona ameweka maneno ambayo huwa yana tafsiri kulingana na wakati husika.

Mathalani Februari 5, 2019 mbunge huyo kama alivyowahi kusema kwamba hupenda kuandika ujumbe unaofikirisha, aliweka katika akaunti yake ya Twitter picha ya saa ya mbao aina ya Kensington Station (789), bila ya kuongeza hata neno moja jambo lililoibua maswali mengi juu ya hatua hiyo.

Miongoni mwa maswali ambayo wadadisi walijiuliza ni kama; Je, alikuwa anamaanisha kwamba muda utazungumza, muda unakwenda, wakati ndio huu au ni suala la muda tu!

Jana Alhamisi Februari 14, 2019 Nape katika ukurasa wake huo aliweka picha ya mwalimu Julius Nyerere akiwa ameketi na Moses Nnauye huku watu wengine wakiwa wamesimama nyuma yao, picha inayoonekana kuwa imepigwa miaka mingi iliyopita.

Chini ya picha hiyo Nape ameandika maneno haya;

Mwalimu. : Musa kuna habari gani huko nyumbani kwetu?

Moses: Mwalimu ziko nyingi sana pengine nianze na.....{mlango unagongwa..}....

Kabla ya ujumbe huo ambao haukufafanua zaidi, siku tano zilizopita aliandika ujumbe mwingine wa mafumbo akitumia njia ya maswali na majibu kati ya baba na mtoto.

Mtoto:- Hivi baba ukubwa au udogo wa mbegu ndio unaoonyesha uharaka wa kuota na kukua kwa mmea??

Baba:- Ndio mwanangu, ukuaji wa mbegu ya mchicha na mbegu ya mkorosho haifanani. Mchicha huota haraka na kutumika na kwisha, mkorosho huchelewa lakini hudumu muda mrefu na ni imara!

Ndipo Mwenyezi-Mungu akamwambia Musa, “Tengeneza nyoka wa shaba, umtundike juu ya mlingoti. Mtu yeyote atakayeumwa na nyoka, akimtazama nyoka huyo wa shaba, atapona.”

Mbunge huyo pia siku za hivi karibuni aliandika ujumbe akisema;  Nyani waliposikia kuwa aliyekuwa akiwafukuza wasile mahindi amekufa, walishangilia sana. Mwaka uliofuata walipata njaa kali maana hakukuwa na mahindi. Ndipo walipogundua kuwa mtu aliyekufa ndiye alikuwa mkulima; Ujumbe-Jifunze kuishi na adui yako, maana anaweza akawa ndiye nguzo pekee ya maisha yako