VIDEO: Michango ya wabunge kuhusu Muungano yamkera Makamba, Ndugai toa neno

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makama wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba akizungumza bungeni alipokuwa akijibu baadhi ya hoja zilizotolewa na wabunge walipokuwa wakichangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira) January Makamba amesema baadhi ya maneno yalikuwa yakitumika ni bungeni wakati wa kuchangia bajeti ya Serikali ya mwaka 2019/2020 ni  ya chuki, kudhalilisha, matusi na kejeli.

Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira) January Makamba amekerwa na maneno yaliyokuwa yakitumiwa na baadhi ya wabunge wakati wakichangia mjadala wa Bajeti ya Serikali ya Tanzania kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni.

Akijibu hoja za wabunge leo Jumanne Juni 25 2019, Makamba amesema namna walivyozungumzia Muungano katika mjadala wa bajeti baadhi ya maneno na lugha iliyotumika hazichangii kujenga nyumba ambayo ni Muungano.

“Kuna baadhi ya maneno humu yametusi, yameudhi na kwa kweli yameleta fadhaa kubwa na mimi naomba kwa heshima ya Bunge na nchi yetu baadhi ya maneno yasiruhusiwe kutumika katika Bunge letu,” amesema.

Amesema baadhi ya maneno ambayo yalikuwa yakizungumzwa ndani ya Bunge yalirejea Bajeti ya Zanzibar, mambo ambayo hayana ukweli kwa sababu yeye alikuwepo.

“Baadhi ya maneno yaliyozungumzwa humu ndani ilirejea bajeti ya Zanzibar kuwa Waziri Mpango (Dk Philip Mpango waziri wa Fedha na Mipango) na Serikali ya Muungano wana roho mbaya, haina nia njema kwa Zanzibar, inahasada, ina wivu, chuki,” amesema.

Pia amesema maneno ya Serikali ya Muungano imegoma kufanya mambo ambayo yataleta maendeleo Zanzibar.

“Kwa hiyo mheshimiwa Spika tusiwatie maneno mdomoni viongozi wa Zanzibar ili kusukuma ajenda zetu . Sisi kama nchi tumeweka utaratibu wa kushughulikia mambo ya muungano,” amesema.

Makamba amesema kuna mbunge alitumia lugha ngumu kwa kumsema Waziri wa Fedha, Serikali na CCM na kwamba anashukuru kwa uvumilivu wa wabunge kwa kutohamaki.

Amesema kilichokuwa kikizungumzwa  ni ujenzi wa barabara kutojengwa kwa hiyo kwa sababu hiyo watu wote walio ndani ya Bunge hilo wana chuki na hasada.

“Kuna masuala mengi ya Zanzibar yanapojitokeza na mchango wa Serikali unapohitajika kuna utaratibu mzuri umewekwa katika kuyawasilisha na kuyafanyia kazi,” amesema.

Amesema wakati wa Serikali ya awamu ya nne kuliwahi kujitokeza tatizo la umeme Pemba lakini lilitatuliwa bila shida, matusi, kudhalilishana kejeli wala matusi.

Makamba amesema Sheria ya mikopo imeletwa kwao wiki iliyopita na katika utaratibu wa kushughulikia.

Amesema litashughulikiwa na taarifa itatolewa ya jinsi inavyoshughulikiwa.

“Naomba utusaidie Bunge lako lisiwe chanzo cha kuweka ufa katika nchi yetu wacha watu wengine wafanye huko nje lakini si humu,” amesema.

Akijibu Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema hawaturuhusu Bunge hilo kuanzisha cheche zinazoweza kusababisha moto ambao utaiunguza nchi na kubakia vipandevipande.

“Tutaongeza umakini katika kusikiliza na kufuatilia kuhakikisha kuwa mambo hayo hayajitokezi tena katika siku zijazo,” amesema.