VIDEO: Mifugo 123,219 kupata chanjo ya kimeta Songwe

Muktasari:

  • Serikali imesema pamoja na mambo mengine imejikita kutoa chanjo kwa mifugo katika wilaya ya Momba ili kutokomeza ugonjwa wa kimeta uliosababisha vifo vinne na wagonjwa 77 katika Kata ya Nzoka.

Dar es Salaam. Serikali imesema chanjo 25,500 zimepelekwa wilayani Momba mkoa wa Songwe kwa ajili ya kuchanja mifugo 123,219 kwa lengo la kutokomeza ugonjwa wa kimeta uliolipuka mwishoni mwa mwaka jana katika kata ya Nzoka.

Hayo yamezungumzwa leo Jumatatu Januari 14, 2019 wakati wa makabidhiano ya magari 10 na pikipiki 35 kwa waganga wakuu na waratibu wa mikoa kwa ajili ya kuongeza kasi ya ugunduzi wa ugonjwa wa TB.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Dk Kheri Kagya amesema tayari baadhi ya mifugo imeshaanza kupewa chanjo ili kudhibiti ugonjwa huo.

“Januari 6 mwaka huu zoezi la kuchanja mifugo lilianza na lengo ni kuchanja 123,219 na mpaka sasa chanjo 25,500 zimeshapokelewa na tunasubiri chanjo zingine ili kuhakikisha mifugo yote inafikiwa na wataalamu wetu ili kutokomeza kabisa ugonjwa huu,” amesema Dk Kagya.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema wizara yake inaendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo kuhakikisha wanatokomeza kabisa chanzo cha ugonjwa huo ikiwemo kuchanja mifugo.

Amesema ni jukumu la sekta ya kilimo kuhakikisha inakabiliana na mlipuko huo lakini pia wizara ya afya kujipanga kupunguza usugu wa dawa kwa wanyama na binadamu, lakini pia kuhakikisha wanyama wanapata chanjo pamoja na kutoa mwongozo kwa matibabu kwa wagonjwa wa kimeta.