Mifuko plastiki marufuku kuanzia Juni

Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuanzia Juni Mosi, itakuwa ni marufuku kutengeneza, kuuza, kuingiza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote.

“Aidha, ifikapo Mei 31, mwaka huu itakuwa mwisho wa kutumia mifuko ya plastiki kubebea bidhaa mbalimbali. Kuanzia sasa tunatoa fursa ya viwanda kubadili teknolojia yao, wauzaji kuondoa mizigo yao au kumaliza kuuza yote na kadhalika,” alisema Majaliwa jana wakati akijibu hoja za wabunge walizozitoa katika mjadala wa bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2019/2020 jana jioni.

Alisema, “Ofisi ya Waziri wa Nchi Makamu wa Rais itajiandaa kutumia kanuni chini ya Sheria ya Mazingira ili kulifanya katazo hili kuwa na nguvu ya kisheria. Tunachukua hatua hii kulinda afya ya jamii, wanyama, mazingira na miundombinu dhidi ya athari kubwa zinazotokana na taka za plastiki.”

Alisema katika kuchukua hatua hizo kuna bidhaa lazima zifungashiwe kwa mifuko ya plastiki, “vifungashio kwa bidhaa hizo havitapigwa marufuku kwa sasa. Katika hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, yatatolewa maelezo ya kina kuhusu katazo hili hasa katika maeneo ya uzalishaji wa viwanda, sekta ya afya na kilimo.”

Mawaziri wajibu hoja

Awali, Serikali kupitia kwa mawaziri wake saba, ilipangua hoja kubwa tisa zilizotolewa na wabunge wakati wa mjadala wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu mwaka 2019/20, likiwamo suala la vibali vya kazi na mazingira magumu ya wawekezaji, ikiahidi kuifumua sheria na sera ya uwekezaji ili kuweka mazingira mazuri ya biashara.

Wakati wa mjadala wa bajeti hiyo iliyowasilishwa Alhamisi iliyopita na kujadiliwa kwa siku nne, wawakilishi hao wa wananchi walihoji pia kuhusu, ajira kwa vijana, umeme na elimu.

Vibali ya kazi

Kuhusu hoja ya wageni kunyimwa vibali vya kazi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde alisema mwenye mamlaka ya kutoa kibali cha kazi ni kamishna wa kazi baada ya kujiridhisha kuwa kazi inayoombwa haina mwenye ujuzi wa namna hiyo ndani ya nchi.

“Anachokifanya kamishna ni kusimamia sheria. Kwa mujibu wa sheria mtu akipeleka maombi ya kibali cha kazi anapaswa apewe ndani ya siku 14, ila kwa sasa vinatoka ndani ya siku saba,” alisema. “Anachokifanya ni kuangalia vigezo vya utoaji vibali kulingana na sheria, akiachia kila mtu aje afanye kazi hapa vijana wetu watakosa ajira.”

Vibali vya kielekroniki

Mavunde aliendelea, “ofisi yetu hivi sasa tumeunganishwa katika mfumo wa utoaji vibali vya kielekroniki vitakavyopunguza urasimu. Hakuna mwekezaji amewasilisha maombi yamekaa miezi sita bila kujibiwa. Akiomba ni ndani ya siku saba anapata kibali alimradi awe amekidhi vigezo vyote.

Alisema kibali kinachotolewa kinaunganishwa na mfumo wa vibali vya kazi na kuishi. Sasa hivi mtu akiomba kibali, kamishna wa kazi atakiona na Uhamiaji wataona, kamishna akimkubalia na Uhamiaji wataona nao watatoa cha kusihi, tutatoka siku saba mpaka siku moja ikiwezekana.”

Ajira na ujasiriamali

Hoja nyingine ya wabunge ilihusu ajira. Katika hilo, Mavunde alisema, “kwanza ni kutoa elimu kwa vijana, waelewe nini maana ya ajira maana wengi wanadhani ajira lazima uwe ofisini. Ajira ni shughuli yoyote halali inayomuingizia mtu kipato. Watu wote hawawezi kupata ajira katika mfumo rasmi, tutakachofanya ni kuelezea fursa zilizopo katika sekta isiyo rasmi itakayowezesha wengi wapate ajira.”

Kuhusu uwezeshaji kupitia mfuko wa uwezeshaji wa vijana alisema, “hadi sasa ekari 217,882 nchi nzima zimetengwa kwa ajili ya shughuli za vijana za ujasiriamali.”

Uwekezaji

Kuhusu kuboresha sera na sheria ya uwekezaji nchini Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angellah Kairuki alisema, “Tayari tumefanya tathmini ya mazingira ya uwekezaji na tumeshabainisha maeneo muhimu yanayohitaji kufanyiwa mapitio ili kuyaboresha.

“Kupitia tathmini hii tutakuja na sera mpya ya uwekezaji ambayo imeanza kufanyiwa mapitio tayari tumeanza mchakato wa kupata timu ya watalaamu kuendesha zoezi hili. Sheria ya uwekezaji nayo pia tutaifanyia marekebisho ili kuondoa vikwazo vilivyopo ikiwa ni pamoja na kuwa na vivutio vipya katika sekta maalumu, upatikanaji wa ardhi kwa ajili ya wawekezaji.”

Elimu

Profesa Ndalichako alisema Serikali imebadilisha mfumo wa wadhibiti elimu ambao utawawezesha kuondokana na kufanya kazi kwa mfumo wa kipolisi.

Alisema Serikali iko makini katika udhibiti ubora wa shule kwasababu inaamini ndio jicho lake kuhakikisha wanafikia malengo.

Umeme

Kuhusu usambazaji wa umeme Vijijini unaofanywa na Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu alisema hadi Julai, 2020 vijiji 9,055 vitakuwa na umeme.

Alisema tangu Julai Mosi, 2016 hadi 30 Machi mwaka huu, vijiji 1,969 vilikuwa vimeunganishwa umeme na kwamba ukichanganya na vijiji ambavyo vilikuwa vimeshapatiwa umeme kabla ya Juni 2016 jumla inakuwa vijiji 6,365 kati ya vijiji 12,268. Alisema hiyo ni sawa na asilimia 52 ya vijiji vyote kwa mujibu wa takwimu za Tamisemi.

Alisema hadi kukamilika kwa mradi huo ambao ni wa miezi 24 Juni 30, 2020, vijijini 9,055 vitakuwa na umeme na 3,213 vilivyobakia taratibu za kuvipatia umeme zimeshaanza kupitia mzunguko wa pili wa awamu ya tatu ya Rea.

Barabara

Naibu Waziri (Tamisemi), Mwita Waitara alisema Serikali imeunda timu ambayo itaangalia mtandao wa barabara nchini lengo likiwa ni kuangalia upya mgawanyo wa fedha za matengenezo na imeunda timu ya kitaifa ambayo itafanya kazi yake na kutoa mrejesho.

Afya

Kuhusu ukamilishaji wa maboma ya afya, Mwita alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18 Serikali imetenga fedha kukamilisha maboma 207 na vituo vya afya 552 vinaendelea kuimarishwa.

Alisema katika mwaka 2019/20 imetenga zaidi ya Sh10 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa vituo vingine vipya 52.

Madiwani na wenyeviti vitongoji

Kuhusu posho za wenyeviti wa vitongoji, vijiji na wajumbe wao, Mwita alisema ni kazi ya kujitolea hivyo wanatakiwa kuwa na kazi nyingi na kwamba posho za malazi na vikao kwa madiwani zitakuwa na viwango sawa kwa halmashauri zote nchini.

Ukimwi

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema Serikali imeanza mchakato wa mabadiliko ya sheria ili kushusha umri wa upimaji wa Virusi vya Ukimwi (VVU) kufikia miaka 15.

Alisema katika kufikia malengo ya asilimia 90 ya upimaji na matibabu wameona changamoto ni kundi la vijana na wanaume.