BADO SIKU 8: Mifuko ya plastiki itakupeleka jela siku saba

Dar es Salaam. Serikali imetoa mbinu ya kusalimisha mifuko ya plastiki ili kuepuka kifungo cha siku saba jela au faini ya Sh30,000 kwa atakayekutwa nayo.

Akizungumza jana katika kikao cha watendaji wote wa Mkoa wa Dar es Salaam kilichoitishwa na waziri wa Mazingira, January Makamba, naibu waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara alisema Serikali inaandaa utaratibu wa kutenga maeneo ya kukusanya mifuko hiyo.

Pia, alisema wanaandaa waraka maalumu kwenda kwa maofisa elimu wa shule za msingi na sekondari watakaoelimisha wanafunzi kuhusu zuio hilo na madhara ya matumizi ya mifuko ya plastiki.

Mwita, ambaye ni Mbunge wa Ukonga alitoa agizo kwa kila mkoa kuanzia ngazi ya kata, kutenga maeneo maalumu yatakayotumika kwa ajili ya watu kusalimisha mifuko hiyo.

Wakati Waitara akitoa maelekezo hayo, Waziri Makamba alieleza mambo matatu ambayo alisema hatapenda yajitokeza katika utekelezaji wa zuio la matumizi ya mifuko ya plastiki litakaloanza Juni Mosi.

Aprili 9, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza Serikali kupiga marufuku matumizi ya mifuko hiyo ifikapo Juni Mosi.

Kabla ya kueleza hayo, Makamba alisema, “Nawaomba niwatoe wasiwasi au uoga wananchi kuhusu zuio hili. Jambo hili lina baraka zote za viongozi wetu wa juu, kusijitokeze wasiwasi, uoga na mashaka, hili ni tamko la Serikali na lazima litekelezwe na kufanikiwa.”

Makamba alisema katika kusimamia sheria na kanuni zilizopitishwa kuhusu zuio hilo, jambo la kwanza ambalo hatarajii lijitokeze baada ya kuanza kwa mchakato ni watu kupigwa virungu.

“Hatutegemei katika zoezi hili kuona kinamama wanabebwa juujuu, au wazee na vijana bali utumike muda mrefu kuelimisha na kuelezana na wale watakaobainika ni wabishi, hapo sheria ichukue mkondo wake.

“Tunategemea baada ya Juni Mosi, watu wasitumie mifuko hii, lakini sitarajii kuona wanamgambo wakiwashika kina mama na kuwapiga virungu endapo wakikutwa na mfuko mmoja au miwili,” alisema Makamba.

Makamba alisema jambo la pili hatarajii kuona watu wakiporwa mali zao baada ya kumkuta mtu na bidhaa hizo, badala yake alipishwe faini.

“Jambo la tatu tutapita kwenye maduka na magenge kuona kama bado kuna matumizi ya mifuko ya plastiki. Hatutegemei kusimamisha watu njiani na kuanza kuwafanyia upekuzi kwenye mifuko yao na mabegi kuona kama wanahifadhi mifuko ya plastiki.

“Ukimuona mtu anatumia hapo anapaswa kuchukuliwa hatua, lakini si kusimamisha magari na kuyapekua au kuingia ndani ya nyumba ya mtu, hapo tutakuwa hatutendi haki,” alisema Makamba.

Makamba alisema fedha zitokanazo na faini za zuio hilo zitabaki kwenye maeneo husika zikiwamo manispaa, Serikali za Mitaa na Baraza la Taifa la Hifadhi ya Mazingira (Nemc) kwa matumizi mengine.