Miili tisa ya Waethiopia yazikwa baada ya kukakaa mochwari miezi mitatu

Muktasari:

Miili ya Waethiopia hao inadaiwa kutupwa na dereva kando ya barabara ya Morogoro-Iringa eneo la Sangasanga

Morogoro. Baada ya miezi zaidi ya mitatu, miili tisa ya raia wa Ethiopia kati ya 13 iliyohifadhiwa Mochwari ya Morogoro imezikwa katika makaburi ya Kola, manispaa ya Morogoro.

Miili hiyo ilihifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Rufaa Morogoro baada ya kudaiwa kutupwa na dereva ambaye kwa sasa anashikiliwa na vyombo vya dola na tayari amefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Morogoro.

Desemba 30 mwaka jana, wahamiaji haramu 26 walitelekezwa kando ya barabara ya Iringa-Morogoro eneo la Sangasanga huku 13 wakiwa wamepoteza maisha na wengine walifikishwa katika hospitali ya mkoa huo kwa matibabu.

Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Steven Kebwe akizungumza wakati wa mazishi hayo, leo Machi 22, 2019, amesema Waethiopia hao walifariki dunia kwa kukosa hewa wakati wakisafirishwa kwenda Afrika Kusini.

Dk Kebwe amesema miili mitano ilichukuliwa na ndugu zao kwenda Ethiopia na taratibu zote za mazishi zimeshafanyika kwa mujibu wa taarifa.

“Tanzania na Ethiopia tutaendelea kushirikiana lakini suala la wahamiaji haramu tutaendelea kuwakamata si kwa Waethiopia tu bali na mataifa mengine ya Ukanda wa Jangwa la Sahara,”alisema.

Kaimu balozi wa Ethiopia nchini, Yonas Yosef Sanbe amesema ameshangazwa na tabia ya vijana Kusini mwa Ethiopia kuwa na tabia ya kutoroka na kusafiri kilometa 1,000 kwenda mpaka na Kenya na kuanza safari ya Afrika ya Kusini.

Amesema kumekuwa na udanganyifu wa watu wanaofanya kazi ya usafirishaji haramu wa binadamu kuwapeleka nchi nyingine kwa madai kuwa huko kuna maisha mazuri kuliko nchini yao.

Sanbe amesema kuna haja ya nchi za Kenya, Tanzania na Ethiopia kufanya mkutano wa pamoja kwa ajili ya uhamiaji unaoendelea na kuona ni namna gani wanaweza kuweka mikakati ya pamoja kudhibiti hali hiyo.

Katika ibada ya mazishi hayo iliyoendeshwa kwa kuzingatia dini mbili, ile ya Kiislamu iliongozwa na Sheikh Abdallah Jafari huku ile ya Kikristo ya dhehebu la Exodus iliendeshwa na Askofu Cleophace Bachuba.

Mazishi hayo mbali na kuhudhuriwa na balozi wa Ethiopia nchini, pia yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ikiwemo idara ya uhamiaji, manispaa na wananchi wa kawaida.