Miili ya watu 60 ajali ya lori la mafuta Morogoro imehifadhiwa mochwari, 70 wajeruhiwa

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa Morogoro, Dk Stephen Kebwe amesema miili ya watu 60 waliokufa baada ya lori la mafuta kupinduka eneo la Msamvu mkoani Morogoro na kuwaka moto muda mfupi baada ya watu kuanza kuchota mafuta hayo imehifadhiwa mochwari.

Dar es Salaam.  Mkuu wa Mkoa Morogoro, Dk Stephen Kebwe amesema miili ya watu 60 waliokufa baada ya lori la mafuta kupinduka eneo la Msamvu mkoani Morogoro na kuwaka moto muda mfupi baada ya watu kuanza kuchota mafuta hayo imehifadhiwa mochwari.

Akizungumza leo Jumamosi Agosti 10, 2019 Dk Kebwe amesema  zaidi ya watu 70 wamejeruhiwa na kupelekwa Hospitali ya Mkoa huo wa matibabu.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Dk Ritha Lyamuya amesema wamepokea miili 60 hadi leo saa 5:30 asubuhi na kwamba bado wanaendelea kupokea mingine.

“Majeruhi tuliowapokea hapa 52 wanaume na wanane ni wanawake. Tumelazimika kuwaomba madaktari na wauguzi kutoka hospitali na vituo vingine vya afya katika manispaa ya Morogoro kwa kuwa leo ni mapumziko,” amesema Lyamuya.

Akizungumzia kuhusu chanzo cha ajali hiyo, Dk Kebwe amesema dereva wa lori alikuwa anakwepa bodaboda na kusababisha lori hilo kupinduka.

“Kwenye lori kulikuwa na watu watatu, dereva na kondakta na mwanamke mmoja. Dereva na huyo mwanamke wamebanwa watu walijitahidi kuwaokoa,” amesema Kebwe.

Amesema baada ya lori hilo kuanguka, mtu mmoja alitaka kuiba betri, wakati akifanya hivyo ukazuka moto na kusababisha maafa hayo.

Tukio hilo limetokea leo ambapo Mwananchi limefika eneo hilo na kushuhudia miili iliyoungua ikiwa imelazwa pembeni ya barabara ya  Dar es Salaam-Morogoro wengi wakiwa ni madereva bodaboda na mamalishe wanaofanya shughuli zao hapo.

Saa 4 asubuhi leo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa amesema karibu watu 57 wamepoteza maisha katika ajali hiyo iliyotokea saa mbili asubuhi.

Ajali hiyo imetokea umbali wa mita 200 kutoka kituo kikuu cha mabasi Msamvu ukitokea Dar es Salaam.

Baadhi ya mashuhuda wamelieleza Mwananchi kuwa baada ya lori hilo kupinduka, watu walianza kuchota mafuta hayo.

Wamesema mmoja wa waliokuwa wakichota mafuta hayo alikuwa akivuta sigara, kwamba ndio chanzo cha mlipuko huo.

Abdallah Msambali amesema aliwaona waendesha bodaboda wakigombania kuchota mafuta kwa kutumia vyombo mbalimbali.

Miili ya waliofariki dunia imeondolewa eneo hilo na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Polisi na Zimamoto na baadhi kupelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.

Leo asubuhi Kebwe wakati akihojiwa na wanahabari amesema, “Haijawahi kutokea maafa makubwa namna hivi Morogoro, lori lilikuwa limepakia mafuta ya petroli lilianguka pembeni mwa barabara hapa Msamvu na kuanza kuvuja mafuta ambayo yalisambaa umbali wa mita 100,” amesema Kebwe.

“Baada ya moto kudhibitiwa tutaangalia maiti nyingine zitakazokuwa zimebanwa na lori la mafuta. Madaktari wote waliopo Manispaa ya Morogoro tumeshawapanga hospitali ya Mkoa kutoa huduma kwa majeruhi, wagonjwa wenye nafuu tutawahamishia wodi nyingine kupisha hii dharura,” amesema Dk Kebwe.

 

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi