Mikakati ya kufikia tani 600,000 ya korosho yabainishwa

Muktasari:

  • Bodi ya Korosho Tanzania imeelezea mikakati mbalimbali inayofanywa ili kuhakikisha uzalishaji wa korosho unafikia tani 600,000 mwaka 2023/24 kutoka tani 313,000 za mwaka 2017/18.

Mtwara. Wakati wakulima wa zao la korosho wakiendelea na maandalizi ya shamba kwa ajili ya msimu ujao, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, Francis Alfred amesema mwaka 2017/18 uzalishaji ulionekana kupanda hadi tani 313,000 lakini katika msimu unaoisha 201/19 uzalishaji umeshuka hadi tani 244,000.

Akizungumza jana Jumatano Juni 12,2019 jijini Mtwara wakati wa mafunzo kwa wakulima alisema jukumu la bodi ni kusimamia korosho kuanzia uzalishaji mpaka sokoni.

Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha uzalishaji unaongezeka ambapo wamekuja na mkakati wa kuandaa mafunzo kwa ajili ya wakulima na maofisa ugani ili kufikia tani 600,000 ifikapo mwaka 2023/24.

“Mwaka 2017/18 uzalishaji ulipanda ukawa tani 313,000 lakini mwaka huu tunaomalizia 2018/19 uzalishaji umekuwa tani 244,000.”

“Kwa hiyo kumekuwa na kushuka kwa uzalishaji, sasa sisi kama bodi ya korosho jukumu letu ni kuhakikisha uzalishaji unaongezeka na lengo la Serikali ni kuongeza uzalishaji wa korosho kutoka tani 313,000 za mwaka 2017/18 kufikia tani 600,000 kwa mwaka 2023/24,”alisema Alfred

Alisema mafunzo hayo yatafanyika kwa vitendo mikoa yote inayolima zao hilo kwa lengo la kuwafundisha wakulima njia sahihi ya kutumia viuatilifu na kuhakikisha ni viuatilifu bora ili kuongeza tija kwa mkulima mmoja mmoja na uzalishaji utakapoongezeka na watu wote katika mnyororo  wa thamani wa korosho watafaidika.

Akizindua rasmi mafunzo hayo, Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa aliwataka wakulima wa korosho mkoani humo kuacha kujibweteka kwa kuwa ndio wazalishaji wakubwa nchini na kutambua ipo mikoa pinzani ambayo imeanza kwa kutumia mbegu za kisasa zilizotokana na utafiti na taasisi ya Naliendele.

Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti  Tari Naliendele, Dk Fortunus Kapinga aliwataka wakulima kuacha mazoea ya kuhudumia shamba kwa mazoea na badala yake watumie elimu wanayopewa na wataalamu.