Mimba shuleni zinawatesa walimu

Muktasari:

Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya wanafunzi waliokatisha masomo kwa sababu ya tatizo hilo katika shule za msingi na sekondari nchini, imeongezeka kutoka takribani 3,000 ya mwaka 2013 hadi wanafunzi 5,033 katika mwaka 2016.

Pamoja na kelele nyingi kuhusu tatizo la mimba shuleni bado linaonekana kuwa sugu.

Kila kukicha kumekuwa na taarifa za wanafunzi wa kike kuacha masomo yao kwa sababu ya mimba.

Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro ni kati ya maeneo ambayo suala la mimba za shuleni linawaumiza vichwa.

Takwimu kutoka Ofisi ya Elimu Sekondari Wilayani humo zinaonyesha kuwa kati ya Januari hadi Septemba mwaka huu, wanafunzi 24 wameshindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya mimba.

Ofisa elimu Sekondari wa wilaya ya Kilosa, Paula Nkane anasema wanafunzi hao wamefukuzwa masomo kwa mujibu wa sheria huku waliowapa mimba wakiendelea kusakwa.

 “Kuna kesi zipo mahakamani, polisi na watuhumiwa wanasakwa. Mimba ni changamoto kwa kweli,” anasema Nkane.

Uchunguzi wa Mwananchi ulibaini kuwapo kwa sababu mbalimbali zinazochangia wanafunzi wa kike kupata mimba shuleni ikiwamo umaskini, umbali mrefu kutoka shule na wengine kuishi kwenye vyumba vya kupanga ‘gheto’.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mazinyungu Ngamba Manegese anasema hata elimu bila malipo kwa kiasi fulani inachangia tatizo la mimba kwa sababu baadhi ya wazazi na walezi wanachukulia poa kwa sababu, hawagharamii elimu.

 “Shuleni kwangu mwaka huu wanafunzi wanne wamepata mimba, utashangaa baadhi ya wazazi na walezi hawastuki wanapoambiwa taarifa hizi mbaya! Wanaona poa tu kwa sababu hawagharamii hivyo hawana hasara,” anasema na kuongeza;

“Tafsiri hii mbaya nia ya elimu bila malipo ni kuwapunguzia mzigo wazazi lakini sio wao kuona hakuna shida hata kama watoto wao wataacha shule.”

Tatizo la mimba pia lipo katika shule ya Sekondari ya Zombo ambako mwalimu mkuu wa shule hiyo,  Masau Nagwagwa anasema wanafunzi watatu wamepatamimba mwaka huu.

“Kwa kweli hili jambo linatuumiza vichwa, ni hasara kubwa mtoto wa kike anapoacha shule kwa sababu ya mimba. Jambo la msingi ni kupata suluhisho tu,” anasema.

Kinachosababisha mimba shuleni

Wanafunzi wa kike waliozungumza na Mwananchi wanasema kuishi kwenye vyumba vya kupanga ni kati ya sababu za ongezeko la mimba shuleni.

“Mfano kule nilikopanga huwa nasumbuliwa sana na vijana kiukweli natamani shule yetu ingekuwa na hosteli niishi shuleni, usumbufu huu wakati mwingine wenzetu wanashindwa, wanajikuta wanapata mimba,” anasema Adelina John, Mwanafunzi wa shule ya Sekondari Ukwiva.

Adelina ambaye ni mkazi wa kijiji cha Nyalanda kilicho umbali mrefu kutoka kijiji cha Ulaya iliko shule  anayosoma amepangishiwa chumba kijijini na anajiendesha licha ya umri wake mdogo.

“Wazazi huwa wanatupatia hela kidogo, unakuta haitoshelezi mahitaji kwa hiyo wakati mwingine inabisi ushinde siku nzima bila kula na mwisho wa wiki inabidi utembee hadi kijijini kufuata, mazingira haya ni magumu,” anasema.

Adelina sio peke yake anayeishi kwenye chumba cha kupanga.Mkuu wa Shule ya Sekondari Ukwiva, Ephata Makele anasema wanafunzi wengi wamepangiwa vyumba mitaani kwa sababu shule hiyo haina hosteli.

“Wale wa mbali wazazi wao wamewapangishia, unakuta hakuna ulinzi dhidi yao, umri wao ndio huo wa kushawishika na wakati mwingine, mazingira magumu kama kukosa chakula yanafanya washawishike haraka,” anasema.

Dada Mkuu wa shule hiyo, Asia Militi anasema kukosekana kwa chakula kwa wanafunzi shuleni nako kunachangia kwa kiasi kikubwa baadhi yao kuangukia kwenye mimba.

“Unakuta mwanafunzi anatoka kijiji cha mbali na hana baiskeli, hadi afike shuleni huko njiani anakutana na mambo mengi, tunaomba kujengewa mabweni,” anasema.

Mwalimu Nagagwa anasema ugumu wa maisha, umbali kutoka shule hadi nyumbani na makundi mabaya ni sababu inayofanya mimba ziendelee kuwepo.

Bodaboda hatari

Mwananchi ilibaini kuwa waendesha bodaboda ni kati ya makundi hatari kwa wanafunzi wa kike hasa wanaotoka mbali.

Wengi wamekuwa wakitumia mwanya huo kuwapatia lifti wanafunzi na mwisho, hujikuta wakiangukia kwenye mahusiano ambayo mwisho wake ni mimba.

“ Hawa bodabdoa ndio wanatuharibia watoto wetu, wanatumia umaskini kama mwanya wa kuwahadaa watoto wetu, dawa hapa ni shule wajenge mabwei tu,” anasema Paskalina Richard mkazi wa kijiji cha Ulaya, Kilosa.

Simulizi ya mimba

Mwanafunzi Anitha Julius (sio jina halisi)anasema kilichomponza kupata ujauzito shuleni ni makundi, umaskini na umbali mrefu kutoka kwao hadi shuleni.

“Wenzangu walinishawishi nimkubalie mvulana aliyekuwa ananitaka kwamba angenisaidie hela za matumizi  kumbe nikapata mimba,” anasema Anitha.

Anitha aliyekuwa anasoma shule ya Sekondari Zombo anasema anatamani kurejea shuleni lakini hawezi kwa sababu, sheria haimruhusu tena.

Mzazi ambaye pia ni mshauri katika masuala ya elimu kwenye kata ya Zombo, Hassan Mbamigwa anasema elimu kwa wanafunzi na mazingira mazuri ya kujifunzia itaweza kumaliza tatizo la mimba shuleni.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Zombo, Ismail Kindaile anasema wanachofanya wao ni kushirikiana na uongozi wa shule kuhakikisha kuwa, sheria inafanya kazi yake.

“Shule ikitoa taarifa tunamtafuta muhusika na kumchukulia hatua ikiwa ni pamoja na kuwapeleka polisi na baadae mahakamani,” anasema.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari ya Ukwiva, Rubanga Mapesi anasema sio mimba, lipo pia tatizo la ndoa za utotoni.

“Mwaka huu mwezi wa sababu wanafunzi wawili wameachishwa shule na kuozeshwa, tunaendelea kufuatilia kesi hii lakini tunaomba ushirikiano toka kwenye uongozi wa vijiji ili tuwapate watoto hawa,” anasema na kuongeza:

Nini kinafanyika?

Mwalimu Nagagwa anasema amefanikiwa kuwashawishi wazazi ili wasaidie kujenga hospteli kwa ajili ya kuwahifadhi wanafunzi.

“Wazazi wameshafyatua tofari 15,000 na tulimuona mhandisi wa majengo toka wilayani alikuja. Kwa sababu wazazi wameshatoa matofari, tunaendelea kusaka wadau ili mwisho wa siku tuokoe watoto hawa,” anasema Nagwagwa.

Ofisa Elimu Nkane anasema katika bajeti ya fedha ya mwaka 2018/2019 suala la ujenzi wa hosteli kwa wanafunzi limepewa kipaumbele.

Mbali na ujenzi wa hosteli Nagagwa anasema wamekuwa wakitoa elimu ya afya ya uzazi kwa kwa wanafunzi pamoja na kuwapima mara kwa mara.

Ofisa elimu Nkane anasema wilaya hiyo imepitisha mpango kwa kila shule kuwa na utaratibu wa kuzungumza na wanafunzi kuhusu suala la miili yao.

“Zipo klabu za wanafunzi wa kike ambazo wasichana hukaa na kujadili namna gani wanaweza kuepuka vishawishi,” anasema.

Nkane anasema kila shule inaye mlezi ambaye amekuwa msaada hasa katika kuzungumza na wanafunzi kuhusu afya zao.

Upimaji mimba mara kwa mara

Mwalimu Manegese anasema wao wamekuwa wakiwapima kila baada ya miezi miwili kwa siku za kustukiza.
“Tumenunua kabisa vifaa na tunafanya vipomo hapahapa shuleni, hii imesaidia sana kupunguza mimba kwa wanafunzi wetu,” anasema.

Anasema mwanafunzi akikutwa na ujauzito hulazimika kumpeleka kliniki ili kuweka ushahidi asije ingizwa mkumbo wa kutoa.

Wizara yaja na mkakati

Mkurugenzi wa Idara ya Watoto katika Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Margaret Mussai anasema tayari wizara imezindua Mpango Mkakati wa Kitaifa wa kuendesha kampeni ya kupiga vita mimba za utotoni nchini.

Kwa mujibu wa wizara hiyo, baadhi ya wanafunzi wanapata mimba kutokana na ukatili unaofanywa nyumbani na ndugu, jamaa na marafiki unaofikia takriban asilimia 60, huku asilimia 40 zinazobaki, watoto wakifanyiwa ukatili shuleni na baadhi ya walimu na viongozi wengine.
Kitaifa, wasichana 27 kati ya 100 wanapata mimba wakiwa na umri chini ya miaka 18, kitendo ambacho ni hasara kwa taifa.