VIDEO: Miradi mitatu ya Rais Magufuli inayomfurahisha Zitto hii hapa

Zitto Kabwe, kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo 

Muktasari:

Zitto Kabwe, kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo na mbunge wa Kigoma Mjini amesema tangu mwaka 2016 hadi 2019, Serikali ya Tanzania imesimamia hoja yake ya kuendeleza miradi yake mikubwa ya ujenzi wa reli, umeme na kununua ndege. Amesema hatua hiyo ni nzuri kwa kuwa inalenga kuikamilisha na si kuja na mambo mapya kila mwaka


Dodoma. Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ameipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa kusimamia utekelezaji wa miradi mikubwa mitatu tangu iingie madarakani Novemba 5 mwaka 2015.

Amesema jambo hilo ni zuri linaonyesha msimamo na nia ya kukamilisha miradi hiyo ya ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), umeme katika Mto Rufiji wa Stiegler’s Gorge na ununuzi wa ndege.

“Kuna jambo tuliweke wazi Serikali imekuwa na msimamo mkali kwenye miradi yake. Tangu bajeti ya kwanza mwaka 2016 kuna mradi wa ujenzi wa reli na ununuzi wa ndege. Bajeti ya pili (2017) fedha za reli ziliongezeka na tukaanza kutenga fedha kwa ajili ya mradi wa umeme,” amesema Zitto.

Zitto ametoa kauli hiyo jana Jumanne Juni 4, 2019 katika mahojiano na Mwananchi wakati akizungumzia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali.

Hata hivyo, amesema changamoto ya miradi hiyo ni kutoingiza fedha katika uchumi na mzunguko wa fedha kuwa mdogo.

Katika bajeti ya Wizara ya Nishati mwaka 2019/ 2020 ya Sh2.142 trilioni, Sh1.44 trilioni zimeelekezwa katika mradi wa kuzalisha umeme Mto Rufiji.

Bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano mwaka 2019/2020 ya Sh4.96 trilioni sawa na asilimia 14.5 ya bajeti nzima ya mwaka 2019/2020 ya Sh33.1 trilioni,  Sh3.62 trilioni ambazo ni takribani robo tatu ya bajeti ya wizara nzima zimeelekezwa kwenye sekta ya uchukuzi ambako asilimia 75 zitatumika kujenga reli ya kisasa (SGR) na kuboresha miundombinu yake.

Wizara hiyo pia imetenga Sh500 bilioni kwa ajili ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) zitakazotumika kukamilisha malipo ya ndege ya pili ya Dreamliner na Bombardier Q400 nne na injini moja ya akiba ya Bombardier. Pia, ATCL itawezeshwa kufanya malipo ya awali ya ununuzi wa ndege mbili aina ya A220-300.

“Ukiangalia bajeti nne za Serikali kuanzia 2016 hadi 2019 utaona kwamba hii Serikali imetatua tatizo la kuja kila mwaka na kitu kipya na kutaka kulitekeleza. Kinachofanyika sasa ni chanya kwa Serikali,” amesema Zitto.

Kiongozi huyo wa ACT- Wazalendo amesema changamoto pekee anayoiona ni miradi hiyo kutoingiza fedha katika uchumi na mzunguko wa fedha kuwa mdogo.

“Hali hiyo inasababisha ukuaji wa uchumi kuingia kwenye matatizo ndio maana huoni watu wakiwa na hali bora wakati fedha zinazoingia katika miradi mikubwa ni nyingi sana.”

“Hiki ni kitu ambacho ni chanya (utekelezaji wa miradi mikubwa), mtu anasema acha nifeli lakini nifanye ninachokiamini,” amesema Zitto.