Miss Tanzania apewa nafasi kushinda Miss World

Tuesday November 27 2018

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Miss Tanzania, Queen Elizabeth Makune amepewa nafasi ya kutwaa taji la Miss World, ambalo fainali zake zinatarajiwa kufanyika Desemba 8, mwaka huu Sanya nchini China.

Katika taarifa yao, mtandao wa GoPageant ambao huelezea na kuchambua mashindano mbalimbali ya urembo duniani, ulimtaja Queen Elizabeth kuwa ni kati ya warembo 15 kati ya 113 wanaoshiriki shindano hilo wanaopewa nafasi kubwa ya kutwaa taji hilo lenye heshima duniani katika masuala ya urembo.

Mrembo huyo ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo cha Uhasibu Tanzania(TIA), alitawazwa kuwa Miss Tanzania Sptemba,8 mwaka huu na hii ni baada ya nyota yake kuanza kung’aa katika shindano la Miss Universe na baadaye Miss Dar.

Wengine wanaopewa nafasi hiyo ni Miss Uganda, Quiin Abenakyo, ambaye naye kama atafanikiwa kupenya huenda wote kwa pamoja wakaipeperusha si tu bendera za nchi zao bali ya Afrika Mashariki.

Mtandao huo pia uliwataja warembo wengine kuwa ni Miss Chile, Anahi Hormazabal, ambaye kama atashinda basi hii itakuwa ni mara ya pili kwa nchi hiyo kuondoka na taji hilo.

Wengine ni na nchi wanazowakilisha kwenye mabano ni Andrea Szarvas (Hungary), Maeva Coucke (Ufaransa), Agata Biernat (Poland), Morgane Theresine (Guadalupe), Anukreethy Vas (India), Solaris Barba (Panama), Elya Nurshabrina (Indonesia).

Pia yupo Taylah Cannon kutoka nchini Australia, Vanessa Ponce (Mexico), Natalya Stroeva (Russia), Dayana Martinez (Puetro Rico) na Shrinkhala Khatiwada (Nepal).


Advertisement