Misuli ya nchi zilizoendelea inavyoumiza bei ya mafuta

Wednesday December 12 2018

 

Kelvin Matandiko
By Kelvin Matandiko
More by this Author

Jumatano ya Desemba 5, mwaka huu Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), ilitangaza kupanda kwa bei za mafuta kwa mwezi Desemba. Tangazo hilo ni sehemu ya taarifa ya mabadiliko ya bei hizo zinazotolewa kila mwezi nchini.

Sababu zilizotajwa na Ewura ni ongezeko la bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mwenendo wa bei za mafuta safi nao umekuwa ukilingana na ule wa mafuta ghafi, ingawa kwa viwango vya mabadiliko hutofautiana kutokana na gharama za kusafisha mafuta ghafi na tofauti ya mahitaji ya petroli, dizeli au mafuta ya taa.

Athari ambazo zimekuwa zikitokana na kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo ni kuongezeka kwa bei za bidhaa na huduma kutokana na ongezeko la gharama za usafirishaji kupitia dizeli na Petroli.

Hata hivyo, bei hizo zimekuwa zikiathiriwa zaidi na kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo katika soko la dunia kwa sababu Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoagiza mafuta kutoka nje.

Hadi jana, takriban asilimia 82 ya akiba ya mafuta yote duniani ilikuwa ikishikiliwa na nchi 15 wanachama wa Shirikisho la Nchi Zinazosafirisha Mafuta kwa Wingi (OPEC) ambazo ni Indonesia Libya, Iran, Iraq, Kuwait, Saudi Arabia, Venezuela, Algeria, Nigeria, Ecuador, Gabon, Angola, DR Congo, Umoja wa Falme za Kiarabu na Guinea ya Ikweta.

Wachambuzi wanasema bei ya mafuta imekuwa ikiathiriwa na siasa za kimataifa kupitia wanachama wa shirika hilo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Wamiliki na Waendesha Vituo vya Mafuta Tanzania (Tapsoa), Tinno Mmasi anasema wanachama hao wamekuwa wakitumia fursa ya migogoro ya kisiasa duniani kujiongezea faida katika biashara hiyo.

Siku moja baada ya kupanda kwa bidhaa hiyo, wadau wa mafuta duniani walikutana mjini Vienna, Austria kujadili namna ya kulinda na kuimarisha bei ya bidhaa hiyo na kubainisha matumaini ya kushuka kwa bei hiyo ifikapo Januari mwakani.

“Mafuta yapo ya kutosha, kinachotokea OPEC ndio wanaamua yauzwe kiasi gani na bei gani, wakizalisha kwa wingi mahitaji yanapungua na ukizalisha kidogo mahitaji yanakuwa makubwa na kusababisha mafuta kupanda bei. Ndiyo maana ya kuungana kwa OPEC ili kudhibiti soko la dunia ili waweze kuzalisha faida kubwa,” anasema Mmasi.

Mmasi anasema jambo jingine linalochagia kupanda kwa bei ya mafuta ni siasa za kimataifa zinazoathiri uchumi wa dunia. Anafafanua akisema migogoro hiyo hutengeza fursa ya kutengeneza faida zaidi.

Anataja baadhi ya migogoro katika siasa za kimataifa inayochagiza OPEC kuathiri bei ya soko la dunia ni vita ya kiuchumi kati ya China na Marekani, Urusi na Marekani.

Makamu wa Rais wa Chama cha Wasafirishaji Tanzania (TAT), Omar Kiponza anahusisha athari za soko la mafuta kutokana na vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa Iran.

Nchi hiyo imewekewa vikwazo mara kadhaa ambapo vya hivi karibuni ni vile vilivyotangazwa Agosti mwaka huu baada ya Marekani kuituhumu Iran dhidi ya urutubishaji wa nyuklia.

Miezi kadhaa nyuma Ewura ilisema kupanda kwa bidhaa hiyo katika soko la ndani kunachangiwa na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji wa mafuta (BPS Premium), kuongezeka kwa muda wa kushusha mafuta bandarini na kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya Dola ya Marekani.

Mahitaji, akiba TPDC

Kiponza anapendekeza Serikali kuwa na akiba ya miezi kadhaa ili kuweza kudhibiti bei pale inapopanda ghafla.

“Japan ina akiba kwa zaidi ya miezi sita, Marekani zaidi ya miaka miwili, hilo limekuwa likiwasaidia kuepuka athari za moja kwa moja kwa wananchi wake, lakini sisi bei ikipanda tunaathirika mara moja,” anasema.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kapuulya Musomba anakubaliana na pendekezo hilo akisema shirika hilo liko katika hatua za awali za ujenzi wa vituo vya mafuta ya akiba hapa nchini, lengo ikiwa kudhibiti athari za kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo kwa mlaji.

Kapuulya anasema akiba hiyo itasaidia kuhimili athari hizo katika soko la ndani kwa kipindi cha miezi mitatu. Shirika hilo limeanza kutafuta viwanja jijini Dar es Salaam, Tanga, Morogoro na Mpanda ili kujenga depoti za mafuta hayo ya akiba kwa makadirio ya wastani wa Dola 500 milioni sawa na Sh11bilioni kwa ajili ya uwekezaji huo.

“Kazi inaendelea na kwa sasa tunafanya ukarabati wa tanki moja la TPDC lililoko ndani ya Tipper (ofisi za Kampuni ya Tipper, Kigamboni) lenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 45,000. Tunategemea robo ya mwaka ujao (Septemba 2019), tutaanza kulijenga, kwa sasa unafanyika upembuzi yakinifu,” anasema.

Kwa mujibu wa Ewura, mahitaji ya mafuta ya dizeli kwa siku ni wastani wa lita milioni tano, petroli lita milioni nne huku mafuta ya taa yakitumika kwa wastani wa lita 60,000.

Kwa kutumia msingi wa takwimu hizo za mahitaji ya siku, akiba ya miezi mitatu kwa mafuta ya dizeli itakuwa ni wastani wa lita milioni 300, petroli lita milioni 240 na mafuta ya taa lita 360,000.

Msemaji wa Ewura, Titus Kaguo anasema akiba iliyopo sasa ni wastani wa lita milioni 70 (petroli) zinazoweza kutumika kwa siku 21, mafuta ya ndege yatakayohudumia siku 33 zijazo, dizeli wastani wa lita milioni 100 kwa siku 20 zijazo na mafuta mazito kwa siku 70 zijazo.

Advertisement