Mitazamo ya Dk Bashiru, Polepole na ushindi wa CCM

Homa ya uchaguzi inazidi kupanda ndani ya vyama vya siasa. Mazungumzo na mikakati ya vyama hivyo kwa sasa inaelekea ama kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa au Uchaguzi Mkuu wa 2000.

Hayo yamejitokeza katika “ziara ya kimkakati” ya Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally mkoani Kilimanjaro ambayo ililenga kuhakikisha chama hicho kinateka mitaa na majimbo yote katika uchaguzi wa mitaa na uchaguzi mkuu wa mwakani na kupata ushindi wa kishindo.

Ushindi “wa kishindo” anaozungumzia Dk Bashiru, pia ulizungumzia hivi karibuni na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kuwa chama hicho tayari kimejihakikishia kutokana na idadi kubwa ya wanachama kilionao na miradi mikubwa ya maendeleo inayoendelea kujengwa nchini.

Polepole aliwaeleza wanahabari kuwa “CCM ina wanachama 15 milioni wakati wapigakura mwaka 2020 wanatarajiwa kuwa milioni 21. Tukisema wakapige kura wana CCM pekee kwa wastani wa chini tutapata ushindi wa kishindo wa zaidi ya asilimia 71.

“Tukisema tufanye kampeni za kawaida kabisa kila wanachama watatu wakatafute mpiga kura mmoja tutakuwa na wapiga kura milioni 20. Hii ina maana ushindi utakuwa wa zaidi ya 90.

Lakini Dk Bashiru akiwa Kilimanjaro anasema “hatuwezi kukaa tukasema tutashinda kwa kishindo, uchaguzi ni watu, na ili watu wa kupiga kura wapatikane, ni lazima wajiandikishe.”

Hivyo, katibu mkuu anasisitiza viongozi wa chama hicho kuhakikisha wanapita nyumba wa nyumba, kitanda kwa kitanda na shuka kwa shuka, kuhamasisha watu kujiandikisha muda utakapofika.

Katika ziara hiyo, Dk Bashiru alitembelea wilaya zote za Kilimanjaro na kufanya vikao vinane akisisitiza wananchi kuchagua viongozi wanaotokana na chama hicho. Pia aliwaonya viongozi waliopo aliodai wanakipa chama wakati mgumu.

Kero za wananchi

Ili kufikia malengo hayo, mbali na kujiandikisha kwa wingi, Dk Bashiru anasema pia utatuzi wa kero za wananchi utakisaidia chama kupata ushindi.

Anawataka viongozi wote wa chama na serikali kuhakikisha wanafuata nyayo za Rais Magufuli kusikiliza na kutatua kero za wananchi. “Rais Magufuli hawezi kusimama peke yake kutatua kero za wananchi, amewachagua na kuwateua wakuu wa wilaya, mikoa na mawaziri ili kumsaidia kuhakikisha kero za wananchi zinatafutiwa ufumbuzi, sasa ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha hili linafanikiwa,” anasema.

“Mimi mwenyewe nikiwa ofisini, nina siku ya kusikiliza kero za wananchi, na huwa siondoki hadi waishe hata kama ni usiku, sasa niwatake na ninyi wakuu wa wilaya, wakurugenzi, wakuu wa mikoa na makatibu wa chama wilaya na mikoa kutenga siku ya kusikiliza kero na wananchi waifahamu,” alisema.

Alisema miongoni mwa kero zinazowakabili wananchi ni migogoro ya ardhi, ndoa na mirathi, ajira na kazi, kodi, biashara na uwekezaji, masuala ya kisiasa na huduma za kijamii na miundombinu.

Wabunge mabubu, watoro

Dk Bashiru anaamini ushindi wa kishindo pia si jambo rahisi kama huna viongozi wanaowajibika au wasiokwenda majimboni, akisema hao wasahau uteuzi kwa kuwa wanakipa chama wakati mgumu.

Anamtaja mbunge mmoja mkoa wa Kilimanjaro kupitia CCM kuwa bungeni anahudhuria kwa kiwango ambacho spika hawezi kumfukuza, lakini jimboni kazembea.

“Wabunge wasiokwenda majimboni wasahau uteuzi wa CCM. Tutakwenda hadi kwenye michango yao, kwa kuwa wabunge wengine ni mabubu, wanakaa tu utafikiri amekodi kiti kwenye Bunge. Lazima tuwajibishane,” anasema Dk Bashiru. Alisema kwa sasa wameshakubaliana kwenye kamati kuu na halmashauri kuu, viongozi wote wa kuchaguliwa wa CCM wafanye mikutano, ziara na kutatua kero za wananchi.

“Hili ni jambo la lazima na si hiari. Tutawafuatilia, tutawakagua na wakati ukifika tutaanika mkeka; umefanya mikutano mingapi kwa miaka mitano, ziara mara ngapi, umetatua kero ngapi na umetekeleza ahadi zako kwa kiasi gani kwa?“Tusije tukalaumiana, na siku hizi teknolojia inaruhusu popote nilipo kujua Same wamekusanya kiasi gani cha fedha na kiasi gani kimetumika, na kila mbunge ana rekodi kwenye mfumo na ninauona kwenye simu yangu,” anasema.

Alisema hawawezi wakaaminiwa na umma kuongoza nchi, kutekeleza miradi ya maendeleo halafu wakazembea.

“Bungeni utakuwa na Spika ambaye ni mjumbe wa kamati kuu, na majimboni atakuwa Bashiru na tutalinganisha wakati ukifika,” alisema.

Afunga ‘mitambo’

Akihitimisha ziara katika Wilaya ya Same, Dk Bashiru alisema tayari ameshafunga mitambo mkoa mzima wa Kilimanjaro hivyo wapinzani wasubirie kulipukiwa na mitambo hiyo.

“Nikiwa Hai nilisema nina-test mitambo, sasa nawaambia tayari nimeifunga mitambo Kilimanjaro, na nimehakikisha inafanya kazi vizuri, wasubiri kulipukiwa, kwani mitambo ya kushambulia imeshasimikwa,” alisema Bashiru.

Wagombea wasiofaa

Katika mkuu anazungumzia pia mchakato wa uteuzi wa wagombea, akiwataka wenye mamlaka kuacha kufanya uteuzi kwa kuangalia, undugu, urafiki, ukabila, dini au rangi.

Alisema ni jukumu la viongozi, kuhakikisha wanawateua wagombea safi, wasiopenda rushwa na watakaowatumikia wananchi na kutatua kero.

“Awe na rekodi ya utumishi kwenye eneo lake na mzalendo ambaye atakuwa tayari kutetea serikali yake, chama chake na viongozi wake na nchi yake. Na tukumbuke tutakuwa tunashindanisha wagombea wetu na wale wa vyama vingine vya upinzani.

“Akijitokeza mtu wa aina hiyo, viongozi wa uteuzi mpeni nafasi hata kama anashindana na ndugu yako kwani uchaguzi ni kutafuta kiongozi, siyo mjomba wala shangazi”

Zaidi ya hayo, anawataka wananchi kuwanyima kura wagombea walevi na wasio na sifa.

“Mimi nashauri, akiteuliwa mlevi hata kama ni wa CCM, mmnyime kura. Tumnyime kura kabisa kabisa kama hana sifa, kwani hakuna sababu ya kuletewa watu wasio na sifa.

Dk Bashiru anawaonya makada wa chama hicho, wenye nia ya kugombea ubunge, kuacha kujipitisha makanisani na misikitini kuomba kura.

“Chama hakijatangaza uchaguzi wa wabunge, wale wanaotaka kugombea, acheni tabia za kwenda misikitini na makanisani kutafuta kura, huko mnatakiwa kwenda kuchoma dhambi zenu,” anasema Dk Bashiru.

“Nasikia kuna baadhi ya wagombea wamekuwa wakarimu kuliko wakati wote, kwenye misiba wapo, kwenye mahafali wapo, kipaimara wapo, halafu wanaanza kutangaza, sahani hizi zimeletwa na fulani, jamvi hili limeletwa na fulani, wacha kujipendekea.

Kushawishi wenye sifa

Msomi huyo wa siasa, anawataka viongozi wa chama hicho kuanzia ngazi ya mashina hadi mkoa, kuanza kujipanga kuwashawishi watu wenye sifa za uongozi kuchukua fomu kwenye chama hicho.

Lakini pia anawaonya wenye mamlaka na uteuzi kutenda haki na iwapo watagundulika kuwa wanakiharibia chama au uchaguzi watakiona cha moto.

“Tumeweka mfumo wa taarifa wa kujua kinachoendelea nchi nzima, tunataka tuendeshe uchaguzi safi katika nchi hii. Tusitafutane ubaya mliomba kazi hizi wenyewe,” alisema.