Miundombinu chakavu inavyopoteza mabilioni ya fedha katika maji kila mwaka

Wednesday January 16 2019

 

By Kelvin Matandiko Mwananchi [email protected]

Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa) hupata hasara ya wastani wa Sh350 milioni kila siku kutokana na upotevu wa lita milioni 210 zinazomwagika mtaani katika jiji hilo.

Hasara hiyo inatokana na ukweli kwamba, bei elekezi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kwa lita 1,000 za maji ni Sh1,663 hivyo kwa lita milioni 210 ni sawa na wastani wa Sh350 milioni.

Katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika Dar es Salaam, Desemba 23, mwaka jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mhandisi Cyprian Luhemeja anasema asilimia 42 ya lita milioni 502 zinazozalishwa kila siku hupotea kutokana na miundombinu chakavu ya mabomba inayoshindwa kuhimili msukumo wa maji yanayosambazwa mtaani kupitia vyanzo vyake vinne.

Vyanzo vya uzalishaji wa maji kwa ajili ya kulisha jiji la Dar es Salaam na Pwani kutoka mamlaka hiyo ni mtambo wa Ruvu Juu (lita milioni 196), Ruvu Chini (lita milioni 272), Mtoni (lita milioni sita) na visima 32 vinavyozalisha lita milioni 28, hivyo kufanya jumla kuwa lita milioni 502 kwa siku.

“Maji yanayosukumwa mtaani ni mengi ila matumizi ni kidogo kutokana na mtandao mdogo wa njia za kusambazia. Mabomba yamechoka hivyo matokeo yake yanapasuka kutokana na kuzidiwa na nguvu ya msukumo wa maji, kwa hiyo solution (suluhisho).

ni kufungua njia nyingi ili pressure (msukumo) upungue. Mabomba makubwa hayana mgogoro sana ila haya madogomadogo ndiyo yenye changamoto,” anasema Mhandisi Luhemeja.

Anasema kasi ya kupanuka kwa makazi imekuwa kubwa kuliko ile ya usambazaji wa huduma za maji kwa wakazi wa mikoa hiyo. “Miundombinu iliyopo mtaani ni ileile ya zamani, tunaongelea Tabata, Segerea, katikati ya jiji, Ilala, Kinondoni, Mbezi Beach, Masaki na kwingineko.

Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2014/2015, aliyekuwa Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe alisema makadirio ya kiwango cha maji yasiyolipiwa kwa wakati huo katika Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) kwa miaka mitatu kuanzia 2011-2014 ilikuwa ni asilimia 52 sawa na Sh50 bilioni.

Hata hivyo, takwimu hizo zinaonyesha juhudi za mamlaka hiyo kupunguza kiwango cha upotevu wa maji kutoka asilimia 52 ya mwaka 2014 hadi kufikia asilimia 42 kwa mwaka huu huku lengo likiwa kufikia asilimia 30 mwishoni mwa mwaka wa fedha 2020/2021.

Kutokana na changamoto hiyo, Mhandisi Luhemeja anasema mamlaka hiyo iliamua kutenga Sh40 bilioni kwa ajili ya kuendesha miradi sita ya kusambaza huduma za maji katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.

Miradi hiyo ni Kisarawe-Pugu-Gongo la Mboto (Mei 2019), Jeti-Kitunda-Yombo (Juni 2019), Kimara Tanesco-Bonyokwa (Desemba 2018), Segerea-Kisukulu (Desemba 2018). Pia mamlaka hiyo imekamilisha miradi ya kulaza mabomba eneo la Kiluvya-Kimara Temboni na Salasala.

Pia, kuna mradi mwingine wa kusambaza maji kutoka Chalinze hadi Msoga na miradi midogo katika Wilaya ya Kinondoni.

Anasema hadi kufikia Juni mwaka huu, miradi hiyo itakuwa imekamilika na kufikia wakazi wapatao milioni 1.5 kupitia idadi ya wateja 200,000 wapya.

Hali ilivyo mtaani

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Desemba mwaka jana katika mitaa ya Tabata Kimanga, Mwenge, Kimara na Segerea, umeshuhudia mabomba yakimwaga maji kwa siku kadhaa mfululizo.

Kwa mfano, katika Mtaa wa Mawingu, uliopo Mwenge kulikuwa na mabomba matatu yaliyokuwa yakimwaga maji kwa zaidi ya wiki mbili bila kuonekana na mafundi wa Dawasa ambao huwazuia wateja kutumia mafundi wa mitaani.

Mtaa wa Tabata Kisiwani, kuna bomba lililopasuka na kumwaga maji yenye msukumo mkubwa barabarani kwa zaidi ya wiki mbili.

Meneja wa Mkoa wa Kihuduma wa Dawasa, Tabata, Victoria Masele anasema kutokana na changamoto ya uchakavu wa mabomba, alianzisha utaratibu wa kuyaondoa kwa awamu mabomba hayo na kuweka mapya.

Alisema kwa sasa wako katika awamu ya mwisho ya kuondoa mabomba ya zamani ingawa alisema hana takwimu kamili kiwango walichofikia.

“Mchina (mtandao wa mabomba yaliyowekwa na Wachina) aliweka laini zamani sana ambazo zimekuwa na shida hadi sasa, ni muda mrefu zilikuwa hazina maji, kwa hiyo maji yalipoanza kuja kwa msukumo mkubwa mengi yakaanza kupasuka, tunayabadilisha”.

Kauli ya waziri

Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa aliwaambia waandishi wa habari kwamba, wakati anaingia madarakani Juni, 2018 alikuta mkoa wa Dar es Salaam unaingiza Sh8.2 bilioni kwa mwezi, lakini sasa wamefikia Sh10.1 bilioni na kwamba ongezeko hilo limetokana na jitihada za kuboresha utendaji.

Hata hivyo, alisema licha ya uzalishaji wa maji kuongezeka kiasi cha upotevu wake kimekuwa kikubwa hali inayosababisha yasiwafikie walengwa.

“Sasa tumekuja na utaratibu tofauti, tunataka tuwapime watendaji kutokana na maji yanayouzwa. Mfano, Dar es Salaam leo kwa mwezi tunazalisha lita 12 bilioni lakini mwezi uliopita (Novemba) lita zilizouzwa ni 6.9 bilioni. Lazima tuimarishe kasi angalau tufikie lita 9 bilioni kwa mwezi,” anasema.

Anasema kwamba kwa sasa wizara inaandaa mkataba kwa ajili ya kusimamia mamlaka hizo kwa kuangalia utendaji wake kila baada ya miezi sita ambapo kila mkoa utatakiwa kufikia malengo yatakayopangwa kwa kipindi husika.

Advertisement