Mjasiriamali mdogo auza jumla, rejareja

Thursday January 17 2019Aurea Simtowe

Aurea Simtowe 

By Aurea Simtowe

Uthubutu katika jambo fulani, unaweza kuwa ni mwanzo mzuri wa kukua kiuchumi.

Haijalishi ni magumu mangapi utakayopitia, lakini kutokata tamaa ndiyo jambo litakalosababisha biashara yako isimame na kukua.

Jambo hilo limedhihirika kupitia Loveness Mseke (26) ambaye licha ya kumaliza chuo na kukosa ajira, aliamua kuanza kuuza mafuta ya nyonyo (Castrol oil) ili ajipatie walau fedha kidogo za kuendesha maisha yake.

Anasema mwishoni mwa mwaka jana alinunua mafuta yaliyokamuliwa na kufungasha mwenyewe ili aone faida yake.

“Nilikuwa na mtaji wa Sh70,000; nilinunua mafuta na vifungashio pamoja kisha nikatengeneza nembo ya bidhaa ili kujitangaza zaidi,” anasema.

Anasema lita moja ya mafuta hayo hununua kwa Sh13,000 na anapofungasha katika ujazo wa chupa za Mil 120 hupata kati ya chupa sita hadi nane anazouza kwa Sh6,000 kila moja.

“Mtaji wangu unazidi kukua kila siku na hadi hivi sasa umefikia Sh500,000; ninauza kwa jumla na rejareja.

“Mtu akihitaji kwa jumla kuanzia chupa 10 namuuzia kwa Sh4,000 ili na yeye akapate faida ya Sh2,000,” anasema Loveness.

Anasema masoko ya bidhaa zake anayapata kupitia mitandao ya kijamii kwa sababu mafuta hayo husaidia sana katika ukuaji wa nywele kwa wanawake hivyo wanawake wengi wanachangamkia bidhaa hiyo.

“Katika malengo yangu nataka siku moja niwe na uwezo wa kutengeneza mafuta haya mwenyewe na kuzalisha bidhaa nyingine za nywele ili kuongeza wigo wa watumiaji pamoja na kuzalisha ajira kwa vijana wengi zaidi,” anasema.

“Naangalia ni namna gani naweza kuanza kutengeneza mafuta haya kwa wingi ili niwauzie wengine.”


Advertisement