Mjusi wa Tanzania wa tani 50 aliyepo Ujerumani kurejeshwa

Arusha. Wizara ya maliasili na utalii kwa kushirikiana na Serikali ya Ujerumani ipo katika mazungumzo ya mwisho kurejesha nchini mabaki ya mjusi mkubwa ambaye kitaalam anaitwa Dinosaur aliyekuwa na uzito wa tani 50 ambaye alichukuliwa nchini miaka zaidi 100 iliyopita.

Akizungumza katika hafla ya maandalizi ya safari ya kwenda katika maonyesho ya kimataifa ya utalii nchini Ujerumani (ITB Berlin) ambayo yatafanyika Machi 6 hadi 10, katibu mkuu wa wizara hiyo, Profesa Adolf Mkenda alisema kwamba ujio wa mjusi huyo utakuza kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii nchini.

Alisema kwamba hata hivyo kabla ya kufika nchini mabaki ya mjusi huyo ambayo yameunganishwa kitaalam lazima Jumba la Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam liwe limeboreshwa zaidi.

“Kuna mabaki mengi ya viumbe hao na maliasili nyingine zilizochukuliwa nchini na kupelekwa nchi mbalimbali duniani, hivyo tunajitahidi uhakikisha vinarejeshwa nchini ili watalii waje huku kuona,” alisema.

Alisema kwamba katika kuhakikisha idara ya makumbusho inakuwa na uwezo, wizara hiyo imetoa usimamizi wa baadhi ya maeneo yake kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Wakala wa Misitu nchini ili kukusanya mapato ya makumbusho.

Akizungumzia maonyesho ya Berlin, Profesa Mkenda alizitaka taasisi binafsi na za umma nchini kwenda kushiriki kwa wingi katika maonyesho ya aina hiyo ili kutangaza vivutio na maliasili zilizopo Tanzania.

“Lakini pia tunaita wawekezaji kutoka nchini Ujerumani kuja kuwekeza katika sekta ya utalii hapa nchini,” alisema.

Awali Balozi wa Ujerumani nchini, Dk Detlef Wachter alisema kwamba Serikali ya nchi yake ipo tayari kushirikiana na idara ya Makumbusho ya Taifa ili kumrejesha nchini mjusi huyo ambaye amekuwa akihifadhiwa katika nchi hiyo.

Alisema kwamba ujerumani bado ina imani kubwa na Tanzania katika masuala ya uhifadhi na utalii kutokana na uwapo wa amani na utulivu pamoja na sera nzuri ambazo zinalinda masuala ya uhifadhi.

Akizungumzia maonyesho ya utalii nchini kwake, Balozi Wachter aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kwenda kushiriki kwani ni fursa kubwa kwao kukuza utalii.

Aliongeza kwa kusema kwamba mataifa zaidi ya 180 yatashiriki na kutakuwa na zaidi waonyeshaji 160,000.

“Hii ni fursa nzuri kukuza utalii baina ya Ujerumani na nchi nyingine za Ulaya lakini pia katika maonyesho hayo ambayo ni ya 53 wadau wa sekta ya utalii wataweza kubadilishana uzoefu jinsi ya kukuza sekta hiyo,” alisema balozi huyo.

Ujerumani ni Taifa la tatu kwa kuleta watalii wengi nchini, ambapo kwa sasa kila mwaka zaidi ya watalii 60,000 wanakuja nchini kutoka nchini humo ambao wanaingiza fedha nyingi zaidi kutokana na kukaa kwao nchini muda mrefu tofauti na watalii wa kutoka mataifa mengine.