Mkakati wa ushindi 2020, JPM aondoe kufuli la wapinzani aondoe

Sun Tzu au Master Sun alikuwa Jenerali wa Jeshi la China ya Kale, Karne ya 6 Kabla ya Kristo. Sifa kubwa ya Sun ni uwezo wake mkubwa kimkakati katika medani za kivita. Mawazo ya Sun ndiyo yaliyozalisha kitabu cha The Art of War (sanaa ya vita).

Ndani ya The Art of War, Sun anasema: “Kama unamjua adui na unajijua wewe mwenyewe, huhitaji kuogopa matokeo ya mapambano 100. Kama unajijua wewe lakini humjui adui, kwa kila ushindi utakaopatikana, vilevile utashindwa. Kama humjui adui na hujijui wewe mwenyewe, utapigika katika kila pambano.”

Natumia hekima hii ya Jenerali Sun kumshauri Rais Magufuli kuhusu siasa na Uchaguzi Mkuu 2020. Imebaki takriban miezi 20 Watanzania wachague Rais, wabunge na madiwani ambao wataiongoza nchi kuanzia mwaka 2020 mpaka 2025. Bila shaka Rais Magufuli atagombea muhula wa pili.

Uchaguzi si vita lakini ni mpambano. Na kanuni ya kumjua adui na kujijua wewe mwenyewe inatumika kwenye pambano lolote. Kujijua na kumjua mpinzani inakusaidia kutambua namna ya kujipanga ili kulielekea pambano na kupata ushindi.

Kwa vile Rais Magufuli atagombea urais mwakani, bila shaka wapinzani wake pia watasimamisha mgombea au wagombea. Kwa mantiki hiyo, anahitaji kujijua na kumjua mpinzani wake ili kuwa na mikakati mahsusi ya kupata ushindi. Swali ni je, atajijua vipi na atamjuaje mpinzani?

Kujijua na kumjua mpinzani si kufahamu majina na sura, la! Ni kuelewa kinagaubaga nguvu zake. Swali ni hili, utajuaje nguvu za mpinzani wako kisiasa kama anazuiwa kufanya siasa kwa uwazi?

Nguvu za kisiasa ni namna mwanasiasa anavyowafikia watu na anavyokubalika. Maana watu ndiyo nguvu za wanasiasa.

Tujiulize; utajuaje kama mwanasiasa ana watu au hana bila kumruhusu afanye mikutano ya hadhara? Hapa ndipo mantiki inakuja kuwa Rais anapaswa kuwaacha wapinzani wake wafanye harakati zao za kisiasa ili ajue namna wanavyokubalika au wanavyokataliwa na wananchi.

Aruhusu wafanye mikutano nchi nzima. Hapo ndipo atajua nguvu yao. Mwitikio wa watu kwenye mikutano ya kisiasa utampa picha ni kwa namna gani wapinzani wake wanavyokubalika na wanavyokatalika. Kitakuwa kipimo kizuri kwake kung’amua msuli na mbinu anazopaswa kutumia kushinda uchaguzi ujao.

Wanasema usilolijua ni sawa na giza. Kipindi hiki ambacho mikutano ya kisiasa na shughuli nyingine za wazi za vyama vya siasa zimepigwa marufuku, kutambua kiwango cha kukubalika cha wapinzani wa Rais Magufuli ni sawa na usiku wa giza. Msuli wa vyama vya upinzani hauna mzani kwa sasa.

Kuruhusu shughuli za kisiasa, itamsaidia Rais Magufuli kujua pia msuli wa chama chake. Maana vyama vya upinzani vikifanya mikutano, CCM nayo itaitisha ya kwake. Hivyo, Rais atakuwa na kipindi kizuri cha kutathmini nguvu ya chama chake kujua mbinu atakazotumia kuwakabili wapinzani wake.

Siku hizi mikutano ya kisiasa haifanyiki lakini harakati zimehamia mitandaoni. Wafuasi wa CCM na vyama vya upinzani hurushiana vijembe kwenye mitandao. Kimsingi hicho si kipimo cha kutosha kuonyesha kukubalika kwa vyama. Kuna jamii kubwa ambayo haipo mitandaoni.

Wengine wapo mitandaoni lakini hawapendi kubishana. Unakuta wanaelewa mahali ambako kura zao zinastahili, ila hawasemi kitu kwa sababu hawaamini kama mitandao ni jukwaa sahihi. Ni rahisi kuwaelewa hao kama siasa zitakuwa wazi na vyama kuwa huru kukutana na wananchi na kuzungumza nao.

Uchaguzi Mkuu 2015, takriban watu 15 milioni ndiyo walipiga kura za urais kati ya 23 milioni waliojiandikisha. Kwa mantiki hiyo, watu milioni 8 hawakupiga kura kumchagua Rais.

Idadi hiyo inatosha kufanya uamuzi wowote ukizingatia kuwa Rais Magufuli alipata kura 8.9 milioni na mpinzani wake mkubwa, Edward Lowassa alichaguliwa na watu 6.1 milioni.

Ni dhahiri kuwa kama theluthi ya watu ambao hawakupiga kura, endapo wangemchagua Lowassa, pengine matokeo yangekuwa tofauti. Watu milioni nane ni asilimia 34.8 ya kura zote. Wakati kura alizopata Rais Magufuli mwaka 2015 ni asilimia 38 ya idadi ya watu waliojiandikisha.

Kuna tofauti ndogo mno kati ya idadi ya watu waliomfanya Rais Magufuli kuwa Rais na wale walioamua kubaki nyumbani bila kuchagua. Rais Magufuli alishinda urais kwa kura asilimia 58 ya watu waliopiga kura.

Inapendeza zaidi kuwa na wapigakura wanaozidi asilimia 80 ya waliojiandikisha. Inavutia zaidi Rais kuchaguliwa na zaidi ya asilimia 50 ya watu waliojiandikisha, si zaidi ya asilimia 50 ya waliopiga kura. Zaidi ya asilimia 50 ya waliojiandikisha kupiga kura humaanisha zaidi ya nusu ya watu wenye sifa za kupiga kura kwenye nchi.

Kupitia mikutano, hao watu milioni nane ambao hawakupiga kura mwaka 2015, wanaweza kutoa picha iwapo watapiga kura kwa Rais au upinzani. Na ikiwa wale milioni 8.9 waliomchagua Rais bado wako kwake au wamepungua? Vipi 6.1 milioni waliompa Lowassa, wangapi wamebaki upinzani na wangapi wamebadili imani yao kuelekea CCM?

Mwaka 2020 kutakuwa na zaidi ya milioni nne ya wapigakura wapya. Watoto waliokuwa na umri wa miaka 10 katika sensa ya mwaka 2012, mwakani watakuwa na miaka 18. Wale waliokuwa na miaka 17 mpaka 15 wakati wa Uchaguzi Mkuu 2015, mwakani watakuwa wanaruhusiwa kupiga kura.

Hao wapigakura wapya watakuwa upande gani? Itakuwa rahisi kuwaelewa kama vyama vya siasa vitakuwa huru kufanya siasa na kuona uelekeo wao katika mikutano.

Hivyo basi, nashauri Rais Magufuli aruhusu mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa kama mkakati wake wa ushindi 2020.